Butiama FM Radio

Ajiita Kanali, atapeli laki nne

20 June 2026, 9:39 am

Mzee Thomas James Esore aliejifanya kanali wa jeshi mstaafu na kumtapeli Diwani mstaafu kiasi cha shilingi laki 4 za Kitanzania ili kumpa mwanae nafasi jeshini. Picha na Oscar Mwakipesile

‘Tunaviomba vyombo vya sheria kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kujihusisha na vitendo vya udanganyifu na wizi.“Mwenyekiti wa Mtaa wa Makore, Safari Igembe

Na Oscar Mwakipesile

Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Butiama Wilaya ya Butiama, Richard Mkonasi Kiganga, amedai kutapeliwa kiasi cha shilingi laki nne za Kitanzania na mtu anayefahamika kwa jina la Thomas James Esore,(71) mkazi wa Wilaya ya Musoma,Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alimshawishi Kiganga kwa kujitambulisha kuwa ni Kanali mstaafu wa Jeshi la wananchi (JWTZ) na kwamba angeweza kusaidia kijana wake kujiunga na jeshi hilo kwa kutumia ushawishi wake.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kiganga amesema alianza kupata mashaka baada ya kijana wake kushindwa kuchaguliwa kujiunga na jeshi licha ya ahadi alizopewa. Amesema uchunguzi wake ulibaini kuwepo kwa nyaraka za kughushi, ikiwemo vitambulisho vya NIDA visivyo halali, jambo lililomfanya kugundua kuwa alikuwa ametapeliwa

Sauti ya Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Butiama Wilaya ya Butiama, Richard Mkonasi Kiganga

Kwa upande wake, Thomas James Esore amekanusha kuwa yeye si Kanali wa jeshi kama inavyodaiwa bali yeye ni mkulima huku akikiri kuchukua fedha hizo.

Sauti ya Thomas James Esore

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Makore, Safari Igembe, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.

Sauti ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Makore, Safari Igembe
Barua aliyokutwa nayo mtuhumiwa akisema imetoka makao makuu ya jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ Dodoma. Picha na Oscar Mwakipesile

Igembe amesema lengo ni kubaini mtandao mzima unaohusishwa na vitendo vya utapeli vinavyolenga kuwaingizia hasara wananchi. Aidha, ametoa wito kwa vyombo vya sheria kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kujihusisha na vitendo vya udanganyifu na wizi.