Butiama FM Radio
Butiama FM Radio
30 May 2026, 2:50 pm

‘‘Tulikuwa na uzinduzi wa albamu ya muziki ambayo ilikuwa inafanyika katika sehemu yangu ya biasahara tulimaliza usiku na tulirejea saa tisa usiku tukiwa na mke wangu na kukuta nyumba imechomwa moto” David Wanzagi Nyerere
Na Amos Marwa
Watu wasiojulikana wamevamia nyumba ya Bw. David Wanzagi Nyerere, mkazi wa kitongoji cha Muhunda, Kata ya Butiama, Wilaya ya Butiama, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa kuiba baadhi ya vitu vya thamani pamoja na kuchoma moto nyumba hiyo. Katika tukio hilo, mlinzi wa nyumba hiyo alijeruhiwa na watu hao kabla ya kutekeleza uhalifu wao.
Kwa mujibu wa Bw. Davidi Wanzagi Nyerere, yeye pamoja na mkewe hawakuwepo nyumbani wakati tukio hilo likitokea, kwani walikuwa katika shughuli zao za biashara. Alisema waliporejea nyumbani usiku walikuta nyumba ikiwa imeteketea kwa moto huku mali zote zilizokuwemo ndani zikiwa zimeteketea.
Akizungumzia tukio hilo, shahidi wa tukio James Wanzagi amewataka wananchi kujitafakari kuhusu sababu zinazosababisha matukio ya aina hiyo kujirudia mara kwa mara katika eneo hilo. Amesema kuna umuhimu wa jamii kushirikiana katika kudumisha amani na usalama ili kuzuia vitendo vya uhalifu.
Naye Balozi wa mtaa huo, Yohana Magembe Joackimu, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kufuata sheria na taratibu pale wanapokuwa na malalamiko dhidi ya mtu yeyote. Amesisitiza kuwa kulipiza visasi kwa kuchoma mali za watu si suluhisho na kwamba wahusika wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Wakati huo huo, Bw. Davidi amesema anatarajia kulifikisha suala hilo katika vyombo vya polisi kwa hatua zaidi za uchunguzi.
