Butiama FM Radio

Viongozi, wazazi waaswa kuimarisha malezi na ustawi wa watoto Butiama

14 Aprili 2026, 11:13

 Afisa Tarafa ya Makongoro, Ediga Kiula, akizungumza na viongozi mbalimbali na wazazi waliojitokeza katika maadhimisho ya Maadhimisho ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani yaliyofanyika katika eneo la Makutano, Kata ya Nyankanga. picha na Yunus Himidi

Viongozi wote wa vijiji na vitongoji kwa kushirikiana na wazazi tunapaswa kujua tunao watoto wangapi na kati ya hao ni wangapi ambao wako nje ya mfumo wa elimu ili tuwapeleke shule kwa ajili ya kulinda haki za mtoto”Afisa Tarafa ya Makongoro, Ediga Kiula

Na Oscar Mwakipesile

Viongozi wa ngazi mbalimbali katika Wilaya ya Butiama wameagizwa kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa watoto wasiokwenda shule pamoja na kupambana na ajira za utotoni, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda haki za mtoto.

Agizo hilo limetolewa na Afisa Tarafa ya Makongoro, Ediga Kiula, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani yaliyofanyika katika eneo la Makutano, Kata ya Nyankanga  na kusisitiza umuhimu wa kufanya msako wa watoto walioko nje ya mfumo wa elimu na kuwahamasisha kurejea shuleni

Sauti ya Afisa Tarafa ya Makongoro, Ediga Kiula akitoa maagizo kwa viongozi na wazazi kuhakikisha watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wanarejeshwa katika mifumo ya elimu
Baadhi ya watoto na wazazi waliohudhuria maadhimisho ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani yaliyofanyika katika eneo la Makutano, Kata ya Nyankanga. picha na Yunus Himidi

Aidha, amewataka watoto kuwa watiifu kwa wazazi na walezi wao na kujiepusha na makundi hatarishi yanayoweza kuwapelekea kuingia katika vitendo visivyofaa ikiwemo kujiunga katika makundi ya kiuhalifu.

Sauti ya Afisa Tarafa ya Makongoro, Ediga akiwaasa watotokuwa watiifu kwa wazazi na walezi wao na kujiepusha na makundi hatarishi
Viongozi mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani yaliyofanyika katika eneo la Makutano, Kata ya Nyankanga. picha na Yunus Himidi

Maadhimisho ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani hufanyika kila mwaka yakiwa na lengo la kuhamasisha jamii kutambua changamoto zinazowakabili watoto hao na kuchukua hatua za pamoja kuhakikisha wanapata haki zao za msingi ikiwemo elimu, ulinzi na malezi bora, Kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo: “Tuchukue Hatua Sasa: Linda Haki za Watoto wa Mtaani kwa Maendeleo ya Taifa”, ikisisitiza wajibu wa kila mdau, serikali, wazazi na jamii katika kuhakikisha watoto wote wanaondolewa katika mazingira hatarishi na kurejeshwa kwenye mfumo rasmi wa malezi na elimu.

Wapiga ngoma za asili mkoa Mara maarufu kama Rilandi wakiwaburudisha watu waliohudhuria Maadhimisho ya Kimataifa ya Mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani yaliyofanyika katika eneo la Makutano, Kata ya Nyankanga. picha na Yunus Himidi