Butiama FM Radio
Butiama FM Radio
17 July 2026, 10:25 am

Nimepokea kero na maoni ya wananchi kuhusu huduma za maji, umeme, barabara na ujenzi wa soko la kisasa. Nitazifuatilia kwa karibu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi na wananchi wanaendelea kupata huduma bora.”Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Wilson Mahera Charles
Na Amos Marwa
Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Wilson Mahera Charles, ameendelea na ziara yake ya kikazi katika Kata ya Kukirango kwa kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza kero za wananchi na kuhamasisha utoaji wa huduma za kijamii. Ziara hiyo imeanza kwa kukabidhi vifaa maalum kwa wanafunzi wenye ualbino kupitia Idara ya Elimu ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, kabla ya kufanya kikao na viongozi wa AMCOS kujadili maendeleo ya ushirika, kilimo na masoko ya mazao.
Katika ziara hiyo, Dkt. Mahera pia ametembelea nyumba ya kihistoria ya TANU iliyohusishwa na harakati za Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuelekea Azimio la Arusha. Aidha, alikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kiabakari pamoja na Ofisi ya CCM Tawi la Kiabakari.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Madaraka senta ,Kijiji cha Kiabakari, Dkt. Mahera alisema amepokea kero na maoni ya wananchi kuhusu huduma za maji, umeme, barabara na ujenzi wa soko la kisasa, huku akiahidi kuzifuatilia kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama pamoja na wadau mbalimbali.

Dkt. Mahera amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha huduma za wananchi nchini. Vilevile, amewashukuru viongozi na wananchi wa Kata ya Kukirango kwa ushirikiano na mapokezi mazuri waliompatia wakati wa ziara hiyo.
