Butiama FM Radio
Butiama FM Radio
17 July 2026, 9:54 am

“Nitashirikiana na Serikali pamoja na wananchi kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaohitajika, ili huduma muhimu ziendelee kuwafikia wananchi wa Jimbo la Butiama “Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Wilson Mahera Charles
Na Amos Marwa
Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Wilson Mahera Charles ameendelea na ziara yake ya kikazi kwa kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Kata ya Kyatungwe.
Katika ziara hiyo Dkt. Mahera amekagua barabara ya Sakya–Mayani (Kyatung we–Store), ujenzi wa Zahanati ya Nyamagana unaotekelezwa kwa nguvu za wananchi, Shule ya Sekondari Kyatungwe, kivuko cha Mubisaka pamoja na ujenzi wa matundu 12 ya vyoo katika Shule ya Msingi Kiawazaru.

Mbali na ukaguzi wa miradi hiyo, Mbunge huyo amekutana na wananchi wa Kyatungwe na Kiawazaru ambapo amepokea kero, maoni na ushauri kuhusu huduma mbalimbali za kijamii. Baadhi ya changamoto zilizokuwa ndani ya uwezo wa viongozi wa eneo hilo zimepatiwa ufumbuzi papo hapo, huku nyingine zikichukuliwa kwa ajili ya kufuatiliwa na kutafutiwa suluhisho.

Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Mahera amesema ataendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wananchi kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaohitajika na kwamba huduma muhimu zinaendelea kuwafikia wananchi wa Jimbo la Butiama.
