Butiama FM Radio

Chanjo ya polio awamu ya tatu yazinduliwa Butiama

27 August 2026, 8:34 pm

Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi akizindua zoezi la ugawaji wa chanjo ya polio kwa watoto chini ya miaka 10 iliyofanyika katika Shule ya Msingi Butiama A, Wilayani Butiama. Picha na Amos Marwa

Ninawasihi wananchi wote wa Mkoa wa Mara kuhakikisha watoto wao walio chini ya umri wa miaka 10 wanapata chanjo ya polio, Chanjo hii ni muhimu katika kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa huu na madhara yake, ikiwemo ulemavu.” Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanal Evance Mtambi.

Na Amos Marwa

Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 27 Agosti, 2026 amezindua zoezi la ugawaji wa chanjo ya polio kwa watoto chini ya miaka 10 uliofanyika katika Shule ya Msingi Butiama A, Wilayani Butiama.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mtambi amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa afya ili watoto wote wapate chanjo itakayowakinga dhidi ya ugonjwa wa polio.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, akimpatia mwanafunzi chanjo ya matone ya polio wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto chini ya umri wa miaka 10, lililofanyika katika Shule ya Msingi Butiama A, Wilayani Butiama. Picha na Amos Marwa

 Mtambi amewahakikishia wazazi, walezi na wananchi wote kuwa chanjo hiyo ni salama, haina madhara na inasaidia kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa polio.

Katika awamu hii, jumla ya watoto 1,048,727 wanatarajiwa kupatiwa matone ya chanjo ya polio katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara kuanzia leo tarehe 27 Agosti, 2026 hadi tarehe 30 Agosti, 2026.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Butiama A, Wilayani Butiama, wakishiriki zoezi la utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 10, lililoanza leo, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ulinzi dhidi ya ugonjwa wa polio. picha na Amos Marwa