Butiama FM Radio
Butiama FM Radio
12 September 2026, 7:00 am

“Tumepokea utabiri unaoonesha uwepo wa mvua za wastani hadi juu ya wastani katika Mkoa wa Mara. Hivyo, nawaagiza wajumbe wa Kamati ya Maafa ya Mkoa pamoja na kamati za maafa katika ngazi zote kuhakikisha wanachukua hatua za tahadhari mapema katika maeneo yao, kwa lengo la kulinda maisha ya wananchi, mali zao na mazingira. Aidha, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi ihakikishe inafanya ukaguzi wa migodi yote na kubaini maeneo yenye viashiria vya hatari, ili hatua stahiki zichukuliwe kabla ya madhara kutokea.”Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi
Na Amos Marwa
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi, ameiagiza Kamati ya Maafa ya Mkoa pamoja na kamati za maafa katika ngazi mbalimbali kutekeleza mikakati ya kukabiliana na maafa katika maeneo yao, kwa lengo la kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha.
Akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Mara, Mtambi amesema utabiri unaonesha kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuwa za kiwango cha wastani hadi juu ya wastani, hivyo kuwataka wananchi kuchukua tahadhari mapema kwa kulinda maisha yao, mali na mazingira yanayowazunguka.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameiagiza Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara kufanya ukaguzi katika migodi ya madini, ili kubaini maeneo yenye hatari kwa maisha na mali za wachimbaji, na kuchukua hatua stahiki za kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.
Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya Mkoa wa Mara katika kukabiliana na athari za mvua hizo, kufuatia taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, TMA, inayoutaja Mkoa wa Mara miongoni mwa mikoa inayotarajiwa kuathirika zaidi na hali ya hewa ya El Niño inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa Septemba 2026.
