Butiama FM Radio

BUTIAMA: Watoto chini ya miaka 10 kupata chanjo ya Polio

24 August 2026, 5:42 pm

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Bi. Thecla Mkuchika, ameongoza kikao cha Kamati za Uhamasishaji wa Chanjo ya Polio kilichofanyika tarehe 21 Agosti 2026 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama. Picha na Yunus Himidi

Chanjo hii ya polio imedhibitishwa na mamlaka za afya kuwa ni salama na haina madhara kwa afya ya watoto. Hivyo, tunawaomba wazazi na walezi kuacha imani na dhana potofu kuhusu chanjo hii, badala yake wajitokeze kuhakikisha watoto wao walio chini ya umri wa miaka 10 wanapata chanjo ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa polio.”Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Bi. Thecla Mkuchika

Na Amos Marwa

Wazazi na walezi katika Wilaya ya Butiama wametakiwa kuhakikisha watoto wao walio chini ya umri wa miaka 10 wanapata chanjo ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa polio.

Wito huo umetolewa na Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla Mkuchika, katika kikao cha Kamati za Uhamasishaji wa Chanjo ya Polio kilichofanyika tarehe 21 Agosti 2026 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama wakati wa mafunzo yaliyotolewa kwa wadau wa afya na makundi mbalimbali, wakiwemo viongozi wa dini na maafisa usafirishaji.

Sauti ya mkuu wa Wilaya ya Butiama, Bi. Thecla Mkuchika, akiwamiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo ya polio

Mkuchika amesema chanjo hiyo ni salama na imeidhinishwa na mamlaka za afya, hivyo amewataka wananchi kuacha imani potofu kuhusu chanjo hiyo na badala yake kuhakikisha watoto wanapata kinga dhidi ya ugonjwa wa polio.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Bi. Thecla Mkuchika akielezea usalama wa chanjo hiyo iliyodhibitishwa na wataalamu wa afya
Mmoja wa wadau waliojitokeza katika kikao cha Kamati za Uhamasishaji wa Chanjo ya Polio akitoa maoni yake juu ya elimu hiyo kwenda kwa wazazi na walezi. Picha na Yunus Himidi

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, George Nyamaha, amewaomba wadau waliopata elimu hiyo kuwafikishia ujumbe huo wananchi katika maeneo yao ili kuwahamasisha wazazi na walezi kujitokeza na kuwapatia watoto chanjo hiyo.

Sauti ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, George Nyamaha akiwaomba wadau wote waliohudhuria kikao kuwafikishia ujumbe huo wananchi

Mmoja wa wadau waliojitokeza katika kikao cha Kamati za Uhamasishaji wa Chanjo ya Polio akitoa maoni yake juu ya elimu hiyo kwenda kwa wazazi na walezi. Picha na Yunus Himidi

Chanjo hiyo inatarajiwa kutolewa kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2026, katika vituo vya afya, kaya zote za Wilaya ya Butiama pamoja na maeneo yenye mikusanyiko ya watu, ikiwemo shuleni, makanisa na masokoni,  Wananchi wametakiwa kutumia fursa hiyo kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo kwa ajili ya kujikinga dhidi ya polio.

Sehemu ya wadau mbalimbali waliojitokeza katika kikao cha Kamati za Uhamasishaji wa Chanjo ya Polio kilichofanyika tarehe 21 Agosti 2026 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama. Picha na Yunus Himidi