Butiama FM Radio
Butiama FM Radio
4 September 2026, 1:02 pm

“Nawasihi wananchi wenzangu tuepuke kuuza chakula chote tulichovuna bila kubakiza akiba ya kutosha majumbani. Tusitegemee mazao tutakayoanza kulima kuanzia mwezi Oktoba, kwani hatujui kama yataweza kustawi au kuharibika kutokana na mvua kubwa zinazotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).” Mgendi Kirato, mkazi wa Mtaa wa Makore, Wilaya ya Butiama.
Na Amos Marwa
Wananchi wilayani Butiama wameanza kuchukua tahadhari mbalimbali kukabiliana na uwezekano wa mvua kubwa za El Nino zinazotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), zinazotarajiwa kunyesha katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka huu, Wananchi hao wamesema maandalizi hayo ni muhimu ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza endapo mvua hizo zitakuwa na athari kubwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Butiama FM, wananchi hao wamesema wameanza kuhama maeneo ya mabondeni, kuhifadhi akiba ya chakula pamoja na kusafisha mitaro na maeneo ya kupitisha maji ili kuzuia maji kutuama na hivyo kupunguza hatari ya mafuriko na uharibifu wa mali, Wamesema hatua hizo zinapaswa kuchukuliwa mapema badala ya kusubiri mvua kuanza ndipo hatua za dharura zichukuliwe.
Aidha, wananchi hao wamewataka wanaoishi katika maeneo ya mabondeni kuhamia maeneo salama, huku wakiwasihi wananchi kutouza chakula chote walichovuna na badala yake kuweka akiba ya kutosha kwa matumizi ya baadaye, Wamesema mvua kubwa zinaweza kusababisha mazao yaliyolimwa kuharibika au kufunikwa na maji, hali inayoweza kuathiri upatikanaji wa chakula na kipato cha wananchi.
Kwa upande wa Serikali, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 730 kwa ajili ya kusaidia shughuli za uokoaji pamoja na ukarabati na ujenzi wa miundombinu itakayoweza kuharibiwa endapo mvua hizo zitasababisha maafa, Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza, huku wananchi wakihimizwa kuendelea kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ya mamlaka husika.
