Butiama FM Radio

Wananchi Butiama wahimizwa kusalimisha silaha haramu

15 October 2026, 8:23 am

Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Butiama, ASP Ponsian Rutagandara Kalinjuma akitoa elimu kwa wananchi kupitia kipindi maalumu kinachorushwa na Butiama FM kuhusu kusalimisha kwa hiari silaha haramu kwa muda uliotolewa na wizara ya mambo ya ndani. picha na Oscar Mwakipesile

“Kwa mwananchi ambaye amenunua silaha kutoka kwa mtu mwingine, anatakiwa kwenda kwa wakili mwenye sifa zinazotambulika kisheria ili kuandaliwa mkataba wa mauziano. Baada ya hapo, anapaswa kuwasilisha silaha hiyo katika kituo cha polisi kwa ajili ya uhakiki, ili kuhakikisha anamiliki silaha hiyo kwa mujibu wa sheria,” amesema Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Butiama, ASP Ponsian Rutagandara Kalinjuma

Na Oscar Mwakipesile

Wananchi wa Wilaya ya Butiama mkoani Mara wametakiwa kutumia vyema muda uliotangazwa na serikali wa kusalimisha silaha haramu na kuhakiki silaha zao kwa hiari. Zoezi hilo linafanyika kuanzia septemba mosi hadi Oktoba 31 mwaka huu, kufuatia tangazo lililotolewa na Wiziri ya Mambo ya ndani ya nchi kupitia waziri wake,Patrobas Katambi, likiwa na lengo la kuimarisha usalama na kudhibiti umiliki wa silaha kinyume cha sheria nchini.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Butiama, ASP Ponsian Rutagandara Kalinjuma, wakati akizungumza katika kipindi maalum cha redio cha Butiama FM, ambapo amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kwa kuzingatia muda uliowekwa na serikali. Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa hiyo kwa hiari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za pamoja za kudumisha amani, usalama na utulivu katika jamii.