Butiama FM Radio

MUKIWASA mguu sawa kukabiliana na El Niño

15 October 2026, 8:01 am

Mhandisi Silveri Nziba akizungumza na Butiama FM redio katika eneo la ujenzi wa kingo za mawe katika Mto Kamugegi. picha na Amos Marwa

Lengo la kujenga kingo katika Mto Kamugegi ni kulinda mabomba ya maji yas isombwe na maji wakati wa mvua, ili kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kupatikana kwa wananchi wakati wote wa mvua na baada ya mvua.” Mhandisi Godfrey Businye Charles

Na Amos Marwa

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mugango-Kiabakari (MUKIWASA) imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, kwa kujenga kingo na sakafu katika maeneo hatarishi ili kulinda miundombinu ya maji na kuhakikisha huduma inaendelea kutolewa bila usumbufu.

Akizungumza na Butiama FM redio katika eneo la ujenzi mhandisi Silveri Nziba amesema hatua hizo zinahusisha ujenzi wa kingo za mawe katika Mto Kamugegi, Mfereji wa Busaraga pamoja na maeneo ya mito Nyang’ombe na Ruamugabo, ambayo yamebainika kuwa na hatari ya kuathiri mabomba ya maji kutokana na maji tiririka na mmomonyoko wa ardhi.

Sauti ya Mhandisi Silveri Nziba akizungumza na Butiama FM redio

Kwa upande wake, Mhandisi Godfrey Businye Charles amesema eneo la Mto Kamugegi limekuwa na changamoto kwa muda mrefu wakati wa mvua, hali iliyochangia mabomba ya maji kusombwa na maji yanayotiririka, hivyo ujenzi wa kingo hizo unalenga kulinda miundombinu na kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa wananchi wakati wote wa mvua na baada ya mvua

 Sauti ya Mhandisi Godfrey Businye Charles
 Mhandisi Godfrey Businye Charles akizungumza na Butiama FM redio katika eneo la ujenzi wa kingo za mawe katika Mto Kamugegi. picha na Amos Marwa

Mbali na kuimarisha miundombinu, MUKIWASA imeandaa mabomba ya ziada kwa ajili ya dharura na inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari za kuchukua kabla na wakati wa mvua kubwa, ikiwa ni pamoja na kujiepusha na maeneo hatarishi, ili kupunguza madhara na kuhakikisha usalama wa wananchi pamoja na mwendelezo wa huduma ya maji.

Ujenzi wa kingo za mawe ukiendelea katika Mto Kamugegi. picha na Amos Marwa