Uyui FM
Uyui FM
11 November 2026, 12:50 pm

Uamuzi wa Mahakama Kuu kubatilisha kanuni za adhabu ya viboko shuleni ni hatua ya kulinda haki na utu wa watoto, kwa kuwa kanuni hizo zilikiuka Katiba inayokataza adhabu za kikatili na kudhalilisha.
Na Mohamed Habibu, Samir Salum
Wakili wa kujitegemea mkoani Tabora, Kanani Chombala, amesema uamuzi wa Mahakama Kuu kubatilisha kanuni za adhabu ya viboko shuleni ni hatua ya kulinda haki na utu wa watoto.
Akizungumza na UFR, amesema kanuni hizo zimekiuka Ibara ya 12(2) na 13(6)(e) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazolinda utu wa binadamu na kupiga marufuku adhabu za kikatili na zinazodhalilisha.
Amesema baadhi ya walimu wamekuwa wakiwapiga wanafunzi na kuwasababishia majeraha makubwa, ikiwemo ulemavu, huku akieleza kuwa bado kuna nafasi ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Tabora, Emmanuel Manziriri, amesema wamepokea uamuzi huo na wataandaa kongamano kwa ajili ya kuwapa walimu uelewa kuhusu athari zake katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa manispaa ya Tabora wametoa maoni yao kuhusu suala hilo
Wakili Chombala amewataka walimu kutumia adhabu mbadala zinazojenga tabia njema badala ya viboko, huku akiwahimiza wazazi kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wao.
Uamuzi huo ulitolewa Novemba 3, 2026, ambapo Mahakama Kuu ilibatilisha Kanuni za 2, 3 na 6 za Kanuni za Adhabu ya Viboko za mwaka 2002 baada ya kubaini kuwa zinakiuka Katiba.