Uyui FM
Uyui FM
3 November 2026, 11:11 am

TRA mkoa wa Tabora yaanza kutoa elimu ya kodi na kusajili namba za TIN kwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali, huku ikieleza kuwa zoezi hilo litaendelea katika vyuo vingine mkoani humo.
Na Elson Sabuni
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Tabora imeanza kutembelea vyuo mbalimbali mkoani humo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu masuala ya kodi pamoja na kusajili namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN), kupitia Dawati la Uwezeshaji Biashara.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo -Tabora (AMUCTA), Afisa Kodi wa TRA mkoa wa Tabora, Donata Deogratias, amesema mpango huo utaendelea katika vyuo vingine vilivyopo mkoani humo.
Hata hivyo, amewataka wanafunzi kuzingatia umuhimu wa kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA) pamoja na kutoa ushirikiano ili kurahisisha utoaji wa huduma hiyo.

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa AMUCTA, Paul Sananga, ameishukuru TRA kwa kuwafikia chuoni hapo na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa huduma hiyo kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaohitaji kusajiliwa.
Baadhi ya wanafunzi wa AMUCTA wameeleza kuwa TIN namba itawasaidia kutambulika kama mlipa kodi, kuanzisha na kusajili biashara pamoja na kutimiza baadhi ya mahitaji wakati wa kuomba ajira katika Taasisi mbalimbali.
Kwa mujibu wa TRA mkoa wa Tabora, hatua hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu umuhimu wa namba ya mlipakodi katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.