Uyui FM

TAKUKURU Tabora imeokoa zaidi ya milioni 37.9 katika Kudhibiti ubadhirifu

25 November 2026, 9:09 pm

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tabora, Azza Mtaita. picha na Muhamed Habibu

TAKUKURU Tabora imeokoa zaidi ya milioni 37.9 katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026 kupitia uchunguzi wa rushwa, ubadhirifu na ulinzi wa rasilimali za umma.

Na Muhamed Habibu

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tabora imeokoa jumla ya Shilingi milioni 37,933,644.38 katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, kupitia uchunguzi wa tuhuma za rushwa, ubadhirifu wa fedha na hatua za kulinda rasilimali za umma.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tabora, Azza Mtaita, amesema hayo leo Novemba 23,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema fedha hizo zimepatikana katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Shilingi milioni 21,848,644.38 zilizohusiana na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Choma, Wilaya ya Igunga, wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 683,588,627.

Mafanikio mengine ni kurejeshwa kwa Shilingi milioni 5.8 katika Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) Msisila, Uyui, pamoja na kulipwa kwa Jummanne Saguda Shilingi milioni 2.2 ambazo alikuwa akidai tangu Oktoba 2024 kwa kazi aliyoifanya katika mradi wa TANESCO Mkoa wa Tabora.

Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Tabora. Picha na Muhamed Habibu

TAKUKURU Mkoa wa Tabora imeeleza kuwa katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026 itaendelea kuimarisha elimu kwa umma, ufuatiliaji wa miradi na kudhibiti mianya ya rushwa, huku ikiwataka wananchi kushiriki kikamilifu kutoa taarifa za vitendo vya rushwa.

Sauti ya Mkuu wa TAKUKURU Tabora Azza Mtaita

Baadhi ya wananchi walionufaika na kurejeshwa kwa fedha hizo, Jummanne Saguda na James Lugalila wameishukuru Taasisi hiyo kwa kusimamia haki na kuwasaidia wananchi kupata fedha zao.

Sauti za Wananchi