Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
14 January 2026, 12:55 pm

Mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ni mpango wa serikali unaolenga kuwawezesha kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa kutumia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri (asilimia 4 kwa wanawake, 4 kwa vijana na 2 kwa watu wenye ulemavu). Mikopo hii hutolewa bila riba kwa vikundi vilivyosajiliwa na vinavyokidhi vigezo, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii, kupunguza utegemezi na kuongeza ajira, hasa katika maeneo ya kilimo, biashara na ujasiriamali.
Na Aloycia Mhina
Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imefanikiwa kutoa mikopo ya jumla ya Shilingi bilioni 1.02 kwa vikundi mbalimbali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kipindi cha robo mbili za kwanza za mwaka wa fedha 2025/2026. Mikopo hiyo ni utekelezaji wa agizo la serikali linaloelekeza Halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Akizungumza na Redio Jamii Kilosa, Mratibu wa Mikopo ya Asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Ndugu Jonathani Mlay alisema kuwa katika robo ya kwanza (Julai hadi Septemba), Halmashauri ilitoa mikopo ya Shilingi milioni 541.3, huku robo ya pili ikitoa Shilingi milioni 479 kwa vikundi 38 vinavyoundwa na vijana 13, wanawake 24 na mtu mmoja mwenye ulemavu.
Mlay alieleza kuwa mikopo hiyo hutolewa kwa mujibu wa sheria, ambapo asilimia 4 hupewa vikundi vya wanawake, asilimia 4 kwa vijana, na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.

Alibainisha kuwa mikopo hiyo hupewa vikundi vinavyokidhi vigezo vilivyowekwa, na kwa sasa maandalizi yanaendelea kwa ajili ya utoaji wa mikopo ya robo ya tatu inayotarajiwa kuanza mwezi Januari hadi Machi 2026, ambapo wanavikundi wanahimizwa kuomba mapema ili wanufaike hasa kipindi hiki cha msimu wa kilimo na biashara.
Aidha, Mlay ametoa wito kwa wataalamu wa maendeleo ya jamii katika ngazi ya kata kushirikiana kikamilifu na wanavikundi kuwapa mafunzo na kuwaelekeza namna bora ya kuandaa maandiko ya mikopo ambapo pia alifafanua kuwa Kamati ya Kata inayosimamia mikopo hiyo inaongozwa na Mtendaji wa Kata kama Mwenyekiti, huku Katibu akiwa ni Afisa Maendeleo wa Kata akisaidiana na wataalamu wengine waliopo kwenye maeneo husika.