Pambazuko FM Radio

Timu ya wataalam yaundwa kutekeleza mpango mkakati wa dhana ya Afya Moja

22 May 2023, 1:10 pm

Ugumu umekuwa ukitokea pale kila idara kufanya kazi pekee mfano mtu wa kilimo kutekeleza majukumu yake kwa kuona wakulima wanalima pasi kuangalia uharibifu unaofanyika.

Na Katalina Liombechi

Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na uhifadhi wa wanyamapori Afrika (AWF) kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu, IUCN na wadau wengine wameunda timu ya wataalam kutoka katika bonde la Kilombero kutekeleza mpango mkakati wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu dhana ya Afya Moja.

Timu hiyo imeundwa baada ya warsha na mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika Mei 18 na 19 mwaka huu 2023 katika ukumbi wa TTCIH Ifakara ya kuwajengea uelewa wataalam wa sekta mbalimbali kutoka halmashauri za wilaya ya Malinyi, Ulanga, Mlimba na Mji wa Ifakara kuhusu namna ya kufanya kazi kwa kushirikiana katika kuzuia, kukabiliana na kutatua changamoto za kiafya katika jamii.

Mafunzo hayo yamekuja baada ya changamoto ya kutokuwa na uelewa wa kufanya kazi kwa kushirikiana miongoni mwa wataalamu wa sekta zaidi ya moja.

Awali mganga mkuu kutoka wilaya ya Ulanga Dkt Ally Ramadhan Mjema amesema kumekuwa na magonjwa ambayo chanzo chake kinagusa sekta zingine hivyo mtaalam wa afya kujikuta anatekeleza majukumu ya idara yake kwa kumtibu mgonjwa  na kushindwa kushughulika na chanzo cha ugonjwa

Mganga Mkuu Wilaya ya Ulanga Dkt Ally Ramadhan Mjema {Picha na Katalina Liombechi}
Sauti ya Mganga Mkuu wilaya ya Ulanga Dkt Ally Ramadhan Mjema

Afisa mazingira halmashauri ya Mji wa Ifakara Salome Mayenga amesema ugumu umekuwa ukitokea pale kila idara kufanya kazi peke yake huku akitolea mfano wa mtaalam wa kilimo kutekeleza majukumu yake kwa kuona wakulima wanalima pasi na kuangalia uharibifu unaofanyika.

Afisa mazingira halmashauri ya Mji wa Ifakara Salome Mayenga {Picha na Katalina Liombechi}
Sauti ya Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Salome Mayenga

Hata hivyo wamesema kupitia Elimu waliyoipata itasaidi kutatua changamoto za kiafya kwa kufanya kazi kama timu.

Sauti za baadhi ya wataalamu waliopatiwa mafunzo

Akizungumza katika mafunzo hayo mchumi kilimo na mwenyekiti wa mashirika yasiyo ya kiserikali Kilombero kutoka shirika la AWF Alexander Mpwaga amesema ili kutatua changamoto hiyo wanatarajia kuwa wataalam hao watapeleka mrejesho katika maeneo waliyotoka, kutekeleza maagizo yaliyotolewa na mkuu wa wilaya juu ya kuendeleza shughuli za uhifadhi wa mazingira.

Sambamba na hayo amesema kufanya utekelezaji wa pamoja utasaidia kuzuia athari za kiafya zinazotokana na mwingiliano wa mazingira yanayomzunguka  binadamu, makazi ya wanyamapori pamoja na mimea.

Mchumi Kilimo na Mwenyekiti wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Kilombero kutoka Shirika la AWF Alexander Mpwaga {Picha na Katalina Liombechi}
Sauti ya Mchumi Kilimo na Mwenyekiti wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Kilombero kutoka Shirika la AWF Alexanda Mpwaga

Mkuu wa wilaya ya Kilombero wakili Dunstan Kyobya wakati akifunga mafunzo hayo ameelezea kufurahishwa na kuundwa kwa timu hiyo ijulikanayo KILOMBERO LAND SCAPE ONE HEALTH TECHNICAL WORKING GROUP huku akiwapongeza wadau walioandaa mafunzo hayo na kutoa maagizo kwa wataalam hao kufikisha uelewa kwa jamii kupitia mikutano ya hadhara kwa kuwashirikisha viongozi wa wananchi, wanasiasa na serikali.

Aidha ametoa wito kwa wadau wa mazingira na wataalam kutumia vyombo vya habari kufikisha elimu ya kutosha kwa jamii juu ya dhana ya Afya Moja ili iweze kufanikiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya{Picha na Katalina Liombechi}
Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya