Ileje FM
Ileje FM
19 November 2026, 6:41 pm

Kuezuliwa kwa nyumba hiyo kumepelekea familia hiyo kukosa mahali pa kuishi na kukosa chakula
Na Denis Sinkonde,Mbozi
Mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Mbozi, mkoani Songwe, zimeiacha familia ya Peter Mwashipa katika Kitongoji cha Isela, Kijiji cha Ndolezi, Kata ya Mlangali, katika hali ngumu baada ya nyumba yao kuezuliwa na kuharibu mazao na chakula, hali iliyosababisha familia hiyo kuomba msaada wa haraka kutoka serikalini na kwa wadau mbalimbali.
Familia hiyo yenye watoto watatu wenye ulemavu wa afya ya akili na viungo vya mwili, imeeleza kuwa inakabiliwa na changamoto kubwa ya maisha, huku mvua hizo zikiongeza mzigo wa malezi na mahitaji ya kila siku.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, Peter Mwashipa amesema nyumba yake imeezuliwa upande mmoja, huku chakula na mazao yakiwemo migomba vikiharibiwa na mvua hizo.
Amesema watoto wake wenye umri wa miaka 20, 10 na minne wanahitaji uangalizi wa karibu kwa kuwa hawawezi kujihudumia wenyewe kutokana na hali zao za kiafya, jambo linalomfanya yeye na mke wake kushindwa kufanya shughuli za kawaida za kujipatia kipato.
“Nimewahi kuwapeleka watoto hao katika hospitali mbalimbali kutafuta matibabu bila kupata mafanikio aliyoyatarajia, hali iliyomkatisha tamaa, hivyo kuiomba Serikali na wadau kujitokeza kuwasaidia chakula, matibabu na mahitaji mengine muhimu,” amesema Mwashipa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Isela, Selina Mwenda, amesema familia hiyo inahitaji msaada wa haraka, ikiwemo ujenzi wa nyumba, chakula na mavazi kutokana na mazingira magumu inayokabiliana nayo.
Amesema hali ya watoto hao wenye ulemavu imekuwa changamoto kubwa kwa wazazi wao, ambao wanashindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kawaida za kiuchumi kutokana na muda mwingi kuutumia kuwahudumia watoto hao.
Naye Diwani wa Kata ya Mlangali, David Mboya, akiambatana na wajumbe wa Kamati ya Maafa ya kata hiyo, ametoa pole kwa familia hiyo na kueleza kuwa inahitaji msaada wa haraka kutokana na changamoto za kiafya zinazowakabili watoto hao pamoja na athari za mvua.
Mboya ameiomba Serikali na wadau mbalimbali kujitokeza kuisaidia familia hiyo, akisisitiza umuhimu wa kupatiwa bima ya afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa watoto hao.
Familia hiyo sasa inaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuisaidia ili iweze kupata makazi salama, chakula, mavazi na huduma za afya, wakati ikiendelea kukabiliana na changamoto za malezi ya watoto wenye ulemavu.