Ileje FM

Utapeli kwa njia ya WhatsApp yawaibua Takukuru Songwe

26 May 2026, 4:10 pm

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Songwe, Frida Wikesi, wakati akiwasilisha mafanikio ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.Picha na Denis Sinkonde

Baadhi ya vikundi hivyo hukusanya fedha kutoka kwa wanachama lakini baadaye hugeuka chanzo cha migogoro.

Na Denis Sinkonde,Songwe

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Songwe imetangaza mkakati maalum wa kudhibiti utapeli na wizi wa kidijiti unaofanyika kupitia vikundi vya mitandao ya kijamii (WhatsApp) katika mji wa Tunduma, wilaya ya Momba, Mkoani Songwe.

Hatua hiyo inalenga kulinda fedha za wananchi pamoja na kukomesha utitiri wa vikundi vya kifedha visivyo rasmi vinavyotuhumiwa kuendesha mifumo haramu ya ukusanyaji fedha kinyume cha sheria za nchi katika mkoa huo, hasa mji huo wa mpakani wenye shughuli nyingi za biashara.

Kauli hiyo imetolewa Mei 26, 2026 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Songwe, Frida Wikesi, wakati akiwasilisha mafanikio ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.

Wikesi amesema taasisi imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi waliodhulumiwa kupitia vikundi vya mitandao ya kijamii vinavyojulikana kama vya kusaidiana kimaisha au kufa na kuzikana.

Sauti ya mkuu wa Takukuru mkoa wa Songwe

Amesema baadhi ya vikundi hivyo hukusanya fedha kutoka kwa wanachama lakini baadaye hugeuka chanzo cha migogoro, udanganyifu na dhuluma kwa wananchi waliowekeza fedha zao kwa matumaini ya kupata msaada au faraja wakati wa matatizo.

“Sasa mmeniuliza juu ya vikundi hivi vya kusaidiana vinavyoitwa vya kufa na kuzikana, tumeliona hilo tatizo na tayari tumeshughulikia baadhi ya vikundi baada ya wananchi kuleta malalamiko kwetu,” amesema Wikesi.

Ametoa mfano wa mwananchi aliyefiwa na baba yake ambaye alitarajia kupata mchango wa pole wa zaidi ya Sh milioni mbili kutoka kwenye kikundi chake, lakini alikabidhiwa Sh 500,000 pekee huku kiasi kilichobaki kikiwa hakijarejeshwa hadi sasa, zaidi ya mwaka mmoja tangu tukio hilo kutokea.

“Tunaamini watu wengi wanakumbana na matatizo kama haya, lakini wengine wanaamua kukaa kimya baada ya kudhulumiwa. Tumegundua tatizo hili lipo kwa kiwango kikubwa hasa katika mji wa Tunduma na tumejipanga kulishughulikia,” amebainisha.

Aidha, Wikesi amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa baadhi ya vikundi hivyo haviendeshwi kwa kufuata sheria na taratibu za usimamizi wa vikundi vya kijamii, huku viongozi wake wakibaki madarakani bila uchaguzi wala uwajibikaji kwa wanachama.