Ileje FM
Ileje FM
19 October 2026, 3:34 pm

Ujenzi wa kanisa hilo unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 150 ambapo mpaka sasa wananchi wameshachangia shilingi milioni 5
Na Denis Sinkonde,Ileje
Ileje.Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Abubakar Mussa Kunenge, leo tarehe 18 Oktoba 2026 amemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini, Usharika wa Chabu, mkoani Songwe.
Katika harambee hiyo, RC Kunenge ametangaza ahadi ya Mhe. Waziri Mkuu ya kuchangia shilingi milioni 15, zitakazolipwa mara baada ya kanisa kuwasilisha akaunti kwa ajili ya malipo.
Aidha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe imeahidi kuchangia mifuko 100 ya saruji, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ileje mifuko 50, na Ofisi ya Mkurugenzi mifuko 50, hatua inayolenga kuunga mkono juhudi za kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo ya ibada.
Akisoma risala ya Waziri Mkuu, RC Kunenge amesisitiza umuhimu wa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, huku akiwahimiza kuombea mvua za baraka zisizoleta maafa pamoja na kuiombea amani ya Taifa.
Katika hafla hiyo, RC Kunenge aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Farida Mgomi, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ileje.