Ileje FM

Moto wateketeza hekari 500 za miti Ileje

12 November 2026, 6:22 am

Sehemu ya shamba la miti hekeri lililoungua katika kijiji cha Lali kata ya Ibaba wilayani Ileje.(Picha na Denis Sinkonde)

Kufuatia tukio hilo Mkuu wa wilaya hiyo Wilimani Ndile ameuagiza Wakala wa Misitu Tanzania(TFS) wilaya Ileje kugawa miche ya miti bure kwa wananchi.

Na Denis Sinkonde,Ileje

Moto ambao chanzo chake bado hakijafahamika, ukikolezwa na upepo mkali, umeteketeza kwa nyakati tofauti nyumba tano na mashamba ya miti ya mbao zaidi ya ekari 500 katika Vijiji vya Cheyo, Lali na Shikunga vilivyopo eneo la milimani, Kata ya Ibaba wilayani Ileje mkoani Songwe.

Baadhi ya wananchi wakiwemo waathirika wameeleza kuwa upepo mkali ulikwamisha juhudi za kuuzima moto huo kwa haraka ingawa hatimaye walifanikiwa kuudhibiti, huku wakiomba serikali iharakishe kuwapatia misaada inayohitajika baada ya kaya zao kukosa makazi.

sauti za wananchi

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Bwana Wilman Ndile, akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama, amefika katika eneo hilo na kueleza kuwa serikali imepokea janga hilo kwa masikitiko makubwa na tayari imeanza hatua za kuwasaidia waathirika.

Katika hatua ya awali, Bwana Ndile ameagiza Kamati ya Maafa kufanya tathmini ya haraka ili kubaini ukubwa wa tatizo na kuanza kutoa misaada ya dharura ikiwemo vyakula kwa kaya zilizopoteza makazi.

Mkuu wa wilaya ya Ileje Wilimani Kapenjama Ndile akizungumza wakati wa kukagua eneo ambalo miti imeungua katika kijiji cha Lali wilaya ya Ileje

Ndile ameagiza ifanyike tathmini ya kubaini idadi ya miche inayohitajika ili serikali kwa kushirikiana na wadau wengine iweze kuwapatia waathirika miche mipya kwa ajili ya kurejesha mashamba yao yaliyoteketea.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Ileje

“Nikuagize Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Ileje kuhakikisha barabara katika eneo hilo zinapitika ili wananchi waweze kuvuna miti iliyosalia na kuiuza ili kupunguza makali ya hasara hiyo,” amesema Ndile.