Ileje FM
Ileje FM
28 May 2026, 6:22 am

Inadaiwa kuwa Shizya alichomwa sindano inayodhaniwa kuwa na sumu begani upande wa kushoto, kisha baadaye kuchomwa kisu tumboni upande wa kulia na mke wake, ambaye alitoroka mara baada ya tukio hilo.
Na Denis Sinkonde,Mbozi
Mamia ya wakazi wa kijiji cha Igunda kilichopo Kata ya Mlowo, Wilayani Mbozi mkoani Songwe, wamejitokeza kumzika Shizya Mwangwale (35), aliyefariki dunia baada ya kudaiwa kudungwa sindano ya sumu na kisha kuchomwa kisu cha tumbo na mke wake, Queen Mbuba.
Vilio na simanzi kubwa vimetawala katika makaburi ya Mji Mwema wakati wa mazishi hayo, ambapo majirani na wakazi wa eneo hilo, wakiwemo Vumilia Mwambogolo na Musa Charles, wameonyesha kushtushwa sana na ukatili huo uliofanyika nyumbani kwa marehemu.
Ndugu wa marehemu, Paul Mwaluanda, pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Igunda, Mwambeye Kapesa, wamelaani vikali mauaji hayo na kutoa wito kwa jamii kutatua migogoro ya kifamilia kwa amani badala ya kuchukua hatua za kikatili.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Augustino Senga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa njia ya simu na kueleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa huyo ambaye alitoroka mara baada ya kutenda kosa hilo.