Huheso FM

Elimu itolewe kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya marburg

February 28, 2025, 3:51 pm

Picha Dkt. Raphaeli Kibata Mtaalam wa magonjwa ya mlipuko kutoka Hospitali ya Manispaa ya Kahama

“Elimu bado haifiki kwa wakati kwenye jamii, wataalam wa afya wafike maeneo ya vijijini kutoa elimu, Serikali ibuni namna ya kutoa hamasa kwa wananchi wake”

Na Duah Julius
Mtaalam wa Magonjwa ya Mlipuko kutoka Hospitali ya Manispaa ya Kahama Daktari Raphael Kibata, amewataka Wananchi Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga kuendelea kuchukua tahadhali ya ugonjwa wa Marburg kwa kuzingatia hatua za kujikinga kwa kufuata maelekezo ya wataalam.

Akizungumza Februari 27, 2025 kwenye kipindi cha Darajani, Daktari Raphael Kibata, amesema wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhali zote wanazoelekezwa na Wataalam ikiwemo kunawa mikono na maji tiririka na kuacha kugusana na mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.

Amesema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama ina mwingiliano mkubwa na Wafanyabiashara kutoka mikoa ya jirani hivyo imeendelea kuwakumbusha Wananchi kuchukua tahadhali kwa kuzingatia namna ya kujikinga pindi wanapomuona mtu mwenye dalili ya ugonjwa wa Marburg.

Daktari Raphael Kibata akizungumzia Tahadhali za kuchukua kujikinga na Marburg

Aidha Daktari Kibata ameongeza kuwa Ugonjwa wa Marburg ni hatari na husababisha vifo kwa muda mfupi pindi mtu anapopata maambukizi ya ugonjwa huo kama atakosa matibabu mapema na mpaka sasa hakuna chanjo ya marbaurg.

Daktari Raphael Kibata akiziungumzia matibabu ya mgonjwa wa Marburg

Kwa upande wao wakazi wa Manispaa ya Kahama wakizungumza na Huheso Fm wamesema bado jamii haina uelewa uelewa wa Ugonjwa wa Marburg huku wakiomba Serikali kupitia Mamlaka husika kutoa elimu ya ili kuwasaidia kuendelea kuchukua tahadhari.

Maoni ya Wanananchi jinsi ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu Marburg

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa Kushirikiana na Wadau Wengine Wakiwemo Shirika la Maendeleo ya Habari kwa Redio za Kijamii Tanzania (TADIO) wamekuwa wakitoa matangazo mbalimbali ya kujikinga na Marburg kupitia redio za Kijamii kwa wananchi wa Mkoa Kagera na Mikoa jirani ya Shinyanga, Kigoma, Geita, Mwanza na Mara.