Huheso FM

Cherehani apongezwa kuwezesha mawasiliano, atoa ahadi ya maji

April 7, 2024, 4:30 pm

Mbunge wa jimbo la Ushetu, Emanuel Cherehani akiteta jambo na diwani wa kata ya Ukune

“Mpaka sasa jimbo la Ushetu tunaendelea kulifungua kwa miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara na madaraja kwenye barabara zinazohitaji madaraja hivyo serikali chini ya mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ushetu tunamshukuru kwa kuendelea kutupatia fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo”

Neema Nkumbi-Huheso FM na Huheso digital blog

Wananchi wa kijiji cha Ngokolo katika Kata ya Ukune halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamemwomba mbunge wa jimbo hilo la Ushetu Emanuel cherehani kuungana nao kuhakikisha mradi wa uijenzi wa Zahanati katika kijiji hicho unakamilika.

Wametoa maombi hayo katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa kwa ajili ya kumpongeza kwa kuwezesha upatikanaji wa mnara wa mawasiliano ambapo kijiji cha Ngokolo kilikuwa na changamoto ya mawasiliano kwa wananchi wapatao 2900.

Akisoma risala iliyoandaliwa na wananchi katika mkutano huo kwa niaba ya wananchi, Nyanda Ngatale amesema kuwa changamoto kwa sasa iliyopo kwa sasa ni zahanati kwa ajili ya huduma za afya ambapo wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma.

Sauti ya Nyanda Ngatale mwananchi aliesoma risala kwa niaba ya wananchi wakati wa mkutano wa pongezi kwa mbunge Emanuel Cherehani

Naye kada wa chama cha mapinduzi CCM, Neema Mgeni amewaomba wananchi wa Ushetu hasa wanaume kutokuwabagua katika uongozi wanawake ili kuhakikisha wanainuka kiuchumi huku akiwaasa wanawake wa jimbo hilo kutokuogopa kuomba nafasi za uongozi na wanapopata wakapiganie haki za wanawake.

Amesema katika chama cha Ushirika KACU yupo mwanamke mmoja tu ambaye ni mjumbe hivyo ameuomba uongozi wa ushirika huo kupanua wigo wa kuongeza wanawake katika bodi yao.

Sauti ya Neema Mgheni kada wa CCM akiwaomba wananchi kuendelea kumpa ushirikiano mbunge wa Ushetu, Emanuel Cherehani

Aidha kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Ushetu Emanuel Cherehani amewahakikishia wananchi wa kijiji cha Ngokolo kuwa ukamilishaji wa Zahanati hiyo utafanyiwa kazi ili kusogeza huduma kwa wananchio huku akiwataka kutumia hospitali ya halmashauri ya Ushetu kupata huduma kwa vipimo vyote na tiba zinapatikana hapo.

Sauti ya Mbunge Emanuel Cherehani akizungumza kwenye mkutano wa hadhara huku akiwaahidi wananchi mradi wa maji ziwa Victoria

Hata hivyo mbunge Emanuel Cherehani amesema kuwa mradi wa maji ziwa Victoria upo mbioni kuanza utekelezaji hivyo jimbo hilo linakwenda kuondokana na adha ya wananchi kukumbwa na changamoto ya maji.