Huheso FM

Serikali kujenga shule ya sekondari mpya Ushetu

September 19, 2023, 2:37 pm

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mdeme akichanganya zege la ujenzi wa shule mpya ya sekondari Ulowa halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga

SERIKALI Kuu imetoa Sh milioni 603.8 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika kijiji cha Ngilimba kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Hatua hiyo itawanusuru wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kuelekea shuleni.

Fedha hizo zimetokana na mradi wa uboreshaji wa shule za sekondari (SEQUIP) ambapo zinakuja kwa awamu huku Mkoa wa Shinyanga ikiwa awamu ya pili.

Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme alipoweka Jiwe la Msingi katika ujenzi wa shule hiyo inayotarajia kuanza kuchukua wanafunzi  mwezi Januari mwakani na ipate maji na nishati ya umeme.

Mndeme alimpongeza Adamu Magazi  na familia yake ambao walitoa eneo la ekari 12 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo nakuwapatia serikali ya kijiji  na wazazi wawasomeshe watoto wao.

Diwani wa kata ya Ulowa, Gabriela Kimaro amesema kuna vijiji sita ambapo kulikuwa na shule moja ya sekondari ambapo wanafunzi walilazimika kutumia muda mwingi kwenda shule.