Huheso FM
Huheso FM
9 September 2024, 3:49 pm

“Tukio hili ni kwanza kutokea katika kijiji hiki na hatufahamu kabisa akina nani wamefanya tukio hili na hatumfahamu huyu mtu lakini kwa vile polisi wamefika uchunguzi utafanyika na itajulikana hii ni mara ya kwanza kwa tukio kama hili”
Na Mwandishi wetu John Masolwa-Ushetu
Mwanaume mmoja anaekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 amechomwa moto na watu wasiojulikana katika kijiji cha kundikili Kata ya Ukune Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga.
Tukio hilo limetokea Asubuhi Jumapili September 8, 2024 katika kitongoji cha kundikili mashariki B ambapo mwili wa mwanaume huyo ulikutwa ukiwa tayari umechomwa moto na watu ambao hawajajulikana.
Awali Shuhuda wa tukio hilo ambae pia ni mwenyekiti wa kitongoji jirani na tukio lilipotokea Nkwambi Shiminzi amesema aliona moto ukiwaka pembezoni mwa kijiji hicho nakuamua kwenda kuangalia nini kinawaka na ndipo alipokuta mwili wa mwanaume huyo ukiwaka na kuamua kumpigia simu mwenyekiti wa kijiji cha kundikili.
Nae shuhuda wa pili ambae pia ni mwenyekiti wa kitongoji wa sehemu ambapo tukio limetokea Bundala Malimao ameshindwa kuutambua mwili huo na kwamba marehemu hakuwa mkazi wa kitongoji chake na wala hajui alipo kuwa akiishi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha kundikili Makungu Saidi Shilunga amesema hawatambui watu waliotekeleza tukio hilo na wala hajui sababu ya hao watu kutekeleza tukio hilo katika kijiji chake na kuongeza kuwa tukio hilo ni la kwanza kutokea katika kijiji chake.
Aidha Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na kuuchukua mwili huo kwa taratibu zingine za kiuchunguzi.