Huheso FM
Huheso FM
8 August 2024, 4:01 pm

Jamii katika halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga imetakiwa kuachana na imani potofu zinazochangia uwepo wa unyonyeshaji duni hali inayosababisha utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Kauli hiyo imetolewa na mgeni rasmi ambaye ni diwani wa Kata ya Uyogo, Joseph Bundala akimuwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Hadija Kabojela katika kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshaji yaliyofanyika Agosti 7, 2024 ambapo amewataka wataalum wa afya kuwasaidia akinamama kwa kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kunyonyesha watoto ili kuodokna na udumavu wa akili na mwili.
Awali, akisoma taarifa kwa mgeni rasmi, Afisa lishe wa Halmashauri ya Ushetu Khadija Nasibu amesema katika tafiti walizozifanya hivi karibuni wamebaini kuwa kati ya watoto kumi ni wanne mpaka watano wanaonyonyeshwa ipasavyo na hii ni kutokana na uwepo wa imani potofu kwa baadhi ya jamii, na mtindo wa maisha kuwa mama akinyonyesha mtoto Nyonyo zake zitaanguka/kuelegea
Kwa upande wao baadhi ya akinamama wa Kata ya Uyogo wakizungumza baadaya maadhimisho hayo kwa nyakati tofauti, wamesema vijana wa siku hizi hawazingatii taratibu za afya ya uzazi hali inayosababisha watoto kupata udumavu, kwa kutokunyonyeshwa kwa kipindi cha miaka miwili na pasipo kulishwa vyakula vya makundi yote pamoja na kuhofia mabadiliko ya miili yao.
Hata hivyo, kutokana na matokea ya utafiti wa afya ya uzazi yaliofanyika mwaka 2024 kitaifa imebainika kuwa watoto walionyonyeshwa maziwa ya mama pekee chini ya umri wa miezi sita ni asilimia 64 %, huku utafiti huo ukionyesha kuwa watoto walionyonyeshwa kwa miaka miwili ni asilimia 37%.