Huheso FM

Mifugo yaripotiwa kuuawa kwa sumu za viwanda vya dhahabu

May 8, 2024, 2:17 pm

Mwenyekiti wa baraza la madiwani halmashauri ya Msalala akiongoza kikao

“Mheshimiwa Mwenyekiti kwanza kabisa binafsi kwa hoja hii iliyotolewa hapa kwenye Baraza lako binafsi sijawahi kupata malalamiko hayo sisi kama halmashauri gharama za usajili ni shilingi elfu kumi (10,000) pekee kwa kikundi tutaendelea kufuatilia ubadhilifu huo” Alisema Judica Sumari.

NA NEEMA NKUMBI-HUHESO FM

Madiwani wa halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamelalamikia wawekezaji wa viwanda vya kuchenjua dhahabu kutokuwa na miundombinu iliyobora kulinda mazingira jambo ambalo linapelekea vifo vya mifugo kutokana na kemikali zinazozalishwa kwenye viwanda hivyo.

Malalamiko hayo yametolewa na Diwani wa Kata ya Lunguya Mhe. Benedicto Manuali kupitia kikao Cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo Mei 08, 2024 ambapo amesema kuwa Ng’ombe na Mbuzi wanakufa kutokana na maeneo ya wawekezaji hao kushindwa kuweka uzio ambao utazuia kuingia mifugo hiyo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti tunatambua tunayo migodi kweli na wawekezaji ambao ni chanzo Cha mapato kwa halmashauri yetu lakini Mwenyekiti kuna jambo ambalo ni kero hasa kwa wafugaji baadhi ya wawekezaji wetu hawajajenga uzio kulinda mazingira hii inasababisha mifugo kufa” Alisema Manuali

Akizungumzia suala hilo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mheshimiwa Mibako Mabubu amemuagiza Afisa Mazingira wa Halmashauri kupitia Ofisi ya Mkurugenzi kusimamia na kuendelea kutolea maelekezo yanayostahili kwenye ujenzi wa viwanda hivyo.

Sambamba na hayo Diwani wa viti maalum Mheshimiwa Hamisa Kalinga Ameibua hoja ya Viashiria vya rushwa, Utozwaji wa fedha wakati vijana, wanawake na watu wenye ulemaavu wanapotaka kuunda vikundi ili kukopeshwa na serikali kupitia halmashauri zake.

Akitolea majibu dhidi ya hoja hiyo Afisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya Msalala, Judica J Sumari amesema kupitia Ofisi hiyo wataendelea kufuatilia kwa watumishi ambao wamekuwa wanajihusisha na vitendo hivyo na endapo watabainika hatua Kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.