Huheso FM

Kishimba aomba tiba bure kwa wananchi kama ilivyo kwenye elimu

March 15, 2024, 11:47 am

Picha ya Gari la kubebea wagonjwa lililokabidhiwa katika kituo cha afya Kagongwa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga

”Tunaendelea kuiomba serikali katika swala la matibabu ilitazame kwa jicho la upana sana kuwasamehe watoto shule na matibabu pia iwe bure kwa sababu ni kitu cha lazima” amesema Mbunge Kishimba.

Na Neema Nkumbi- Huheso Fm

Kituo cha afya Kagongwa kinachohudumia wananchi takribani 60,000 wa Kata za Kagongwa, Mondo na Isagehe kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi  ya mwaka 2022 kimepokea gari la kubebea wagonjwa [Ambulance] kwa ajili ya wagonjwa kupata huduma.

Gari hilo limekabidhiwa March 14, 2024 na Mbunge wa Jimbo la Kahama mji Jumanne Kishimba katika hafla ya makabidhiano yaliyofanyika Kata ya Kagongwa Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga, Kishimba amesema kuwa gari hilo limekabidhiwa ili kuokoa uhai wa wananchi hivyo hawana budi kulitunza.

Wananchi wa Kata ya Kagongwa wamesema kuwa kupatikana kwa gari hilo kutasaidia kuokoa uhai wa wagonjwa hasa wanawake na watoto wanao kabiliwa na changamoto nyingi za kiafya.

Sauti ya wananchi wakizungumzia kuhusu gari hilo la wagonjwa lililokabidhiwa kwenye kituo cha Afya Kagongwa

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama Dr Fredrick Malunde licha ya kupokea gari hilo anatambua uwepo wa changamoto ya upungufu wa watumishi kwenye kituo hicho atahakikisha wanaongezeka pindi serikali itakapotoa ajira.

Sauti ya kaimu mganga mkuu hospitali ya Wilaya Kahama, Fredrick Malunde akizungumza wakati wa kukabidhiwa kwa gari la wagonjwa.

Mara baada ya kukabidhi gari hilo mbunge Jumanne Kishimba  amesema changamoto ya matibabu bado ni kubwa ataendelea kumwomba Mheshimiwa Rais Samia kupitia bunge kufanya matibabu kuwa bure kama ilivyo elimu bure kwa sasa.

Sauti ya Mbunge wa Jimbo la Kahama mjini Jumanne Kishimba akizungumza wakati wa kukabidhi gari la wagonjwa katika kituo cha afya Kagongwa