Mikopo ya halmashauri yainufaisha familia ya Mzee Lukuba
January 16, 2025, 12:20 pm
“Awali, wanawake walikuwa wanajiunga na vikundi na kukopa bila kushirikisha waume zao, hali ambayo ilileta migogoro familia kwa familia,”
Na Neema Nkumbi
Familia ya Mzee Lukuba Washa imefanikiwa kujenga nyumba ya kisasa na kununua ng’ombe watano kupitia mikopo ya halmashauri ya asilimia 10, Hii ni baada ya familia hiyo kujiunga na vikundi vya wanawake vya kuweka hisa, ambapo walipata taarifa kuhusu mikopo inayotolewa na halmashauri.
Akizungumza nyumbani kwake wakati wa ziara ya waandishi wa habari, Bi Sophia Emanuel, mke wa Mzee Lukuba, amesema kuwa walianza kwa kuunda kikundi cha wanawake cha kuweka hisa, ambapo walipokuwa wakifanya shughuli za kijamii, walijua kuhusu mikopo ya halmashauri kutoka kwa afisa maendeleo.
Sophia ameongeza kuwa mikopo hiyo imewasaidia sana, hasa kwa kuwa wanafanya shughuli za kilimo kama vile kulima vitunguu, pamoja na kununua mbunga kwa bei nafuu na kuuza kwa bei kubwa, jambo ambalo limewawezesha kurudisha mikopo hiyo bila usumbufu.
Baba wa familia hiyo, Mzee Lukuba, amekiri kuwa awali alipokuwa akisikia kuhusu mikopo ya halmashauri, alijawa na wasiwasi, lakini alikubali mkewe kushiriki kwa sababu aliona faida kwa familia yao, Mzee Lukuba amewashauri wanaume wenzake kuwaachia wake zao kushiriki katika vikundi vya kifedha ili nao wanufaike, kwani vikundi vya aina hii vinasaidia sana.
Kwa upande mwingine, Samwel Samson, kijana kutoka katika jamii hiyo, amesema kuwa wao kama vijana wamehamasishana kuchangamkia fursa za mikopo, na kwamba vikundi vikiwa na vigezo vinavyotakiwa, wanapaswa kupatiwa mikopo bila ubaguzi.
Afisa maendeleo wa kata ya Ngogwa, Ester Sanga, ambaye ni mshauri wa vikundi vya kifedha katika eneo hilo, amesisitiza kuwa kazi yake kubwa ni kuhamasisha jamii kuondokana na mawazo hasi na kujiunga na vikundi ili waweze kupata mikopo ya asilimia kumi ya halmashauri.
Ester ameongezea kuwa mikopo hii siyo kwa wanawake pekee, bali pia kwa vijana na walemavu, na kwamba wanapaswa kujiunga ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.
Mikopo hii ya asilimia kumi ya halmashauri imekuwa na manufaa makubwa kwa familia nyingi, na imechangia kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwapa fursa ya kujenga, kuwekeza katika kilimo, na biashara.