Miaka 15 jela kwa kusababisha kifo akijifanya daktari wa upasuaji
18 August 2023, 6:02 pm
Mahakama kuu kanda yaTabora imetoa hukumu ya kifungo cha miaka kumi na Tano jela kwa Amos Mathias.
Na Salma Abdul.
Amos Mathias mkazi wa Kijiji cha Nhungulu wilayani Nzega amehukumiwa na Mahakama kuu kanda yaTabora kifungo cha miaka kumi na Tano jela baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila kukusudia kwa kujifanya Daktari na kumfanyia upasuaji wa tumbo na sehemu za siri mzee mwenye umri wa miaka 78 Lukwaja Selemani ambaye alikuwa na tatizo la ugonjwa wa mshipa wa ngiri.
Akisoma hukumu hiyo Jaji mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Tabora Athuman Matuma amesema mahakama imepitia hoja za pande zote mbili zilizokubaliana yaani Upande wa Jamhuri na upande wa utetezi kwamba mshtakiwa ni kweli alitenda mauaji hayo pasipo kukusudia.
Awali mshtakiwa Amos aliwatoza ndugu wa marehemu kiasi cha shilingi laki mbili kufanya upasuaji huo ambapo walimpa shilingi laki moja na arobaini na alipoona tatizo limekuwa kubwa aliwapa maelekezo wamkimbize hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi.
Jaji Athuman Matuma ametoa adhabu hiyo ya kutumikia kifungo cha miaka 15 ili kukomesha uovu alioutenda Amos ili hali alikuwa akijua kwamba yeye hana ujuzi wa upasuaji huo uliosababisha kifo cha Mzee huyo.