Uyui FM Radio

Muuguzi aliyetuhumiwa kubaka abainika hana hatia, aachiwa  huru

18 August 2023, 4:58 pm

Muuguzi wa daraja la pili hospitali ya wilaya Sikonge Rayson Duwe akiwa nje ya jengo la mahakama. Picha na Juma Kapipi

Mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Sikonge imemwachia huru afisa muuguzi aliyekuwa akituhumiwa kwa ubakaji baada ya Jamhuri kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo hivyo kuonekana hana hatia.

Na Salma Abdul

Muuguzi wa daraja la pili katika hospitali ya wilaya ya Sikonge ameachiwa huru na mahakama ya hakimu mkazi wilayani humo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake za kumbaka mjamzito aliyekuwa akimhudumia hospitalini hapo.

Akisoma hukumu hiyo hakimu Mkazi wa mwandamizi wa wilaya ya Sikonge Irene Lyatuu amesema kufuatia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha tukio hilo.

Amesema Mahakama imemwachia huru Rayson Duwe kwa sababu hakuwa na hatia iliyothibitishwa pasi na shaka yoyote.

Awali Duwe alikuwa akituhumiwa kwa shtaka la kumchoma sindano ya usingizi mama mjamzito na kisha kumbaka wilayani Sikonge.