Ibada maalumu ya kuliombea Taifa yafanyika Tabora
29 March 2021, 7:13 pm
Waumini wa madhehebu ya kikristo Mkoani Tabora wametakiwa kuendeleza mazuri aliyoyaacha Hayati Dokta John Magufuli ikiwa ni pamoja na kutunza tunu za kitaifa hususani amani, upendo na mshikamano.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora Abel Busalama ambaye alimwakilisha mkuu wa Mkoa wa Tabora Dokta Phillemon Sengati katika ibada maalum ya kuliombea Taifa katika kipindi hiki cha maombolezo ya siku 21.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tazania Dayosisi ya Kanda ya magharibi ya kati KKKT mjini Tabora Daktari Issack Laizer amesema waumini wanapaswa kuendelea kufanya maombi kwa ajili ya taifa ili nchi iendelee kuwa na amani.
Hata hivyo baadhi ya waumini walioshiriki ibada hiyo HELENA KELEKEZA na JOSEPH NGALU ameuomba uongozi wa umoja wa makanisa kuwa na muendelezo wa ibada kama hiyo kwa lengo la kuliombea taifa na mkoa wa Tabora kwa ujumla.
Ibada hiyo maalum ya kuliombea taifa, familia ya hayati Dokta John Magufuli pamoja na watazania kwa ujumla kufuatia kipindi hiki cha maombolezo iliandaliwa na umoja wa makanisa ya mkoani Tabora imefanyika katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tazania Dayosisi ya Kanda ya magharibi ya kati KKKT mjini Tabora.