Radio Jamii Kilosa

Vifo vya mama na mtoto vyapungua Kilosa

14 January 2026, 3:18 pm

Wataalamu wa afya kutoka hospitali ya wilaya ya Kilosa wakizungumza na Redio Jamii Kilosa katika kipindi cha Ijue Halmashauri Yako idara ya Afya. Picha na Beatrice Majaliwa

Uboreshaji wa huduma katika vituo vya afya pamoja na kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kujifungua salama umeelezwa kuwa miongoni mwa mafanikio ya jitihada za serikali katika kuboresha afya ya mama na mtoto wilayani Kilosa.

Na Asha Madohola

Vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi Wilayani Kilosa vimeelezwa kupungua kwa kiwango kikubwa, kutokana na juhudi za utoaji wa elimu ya afya ya uzazi kwa jamii kupitia vituo vya kutolea huduma za afya.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto Wilaya ya Kilosa, Bi. Prisca John, alipokuwa akizungumza na Redio Jamii Kilosa kwenye kipindi cha Ijue Halmashauri yako. 

Bi. Prisca alisema kwa sasa wanawake wengi wameanza kuelewa umuhimu wa huduma za uzazi salama na wanajitokeza mapema kliniki mara tu wanapohisi ni wajawazito, jambo linalosaidia kupunguza hatari wakati wa kujifungua na kwamba desturi ya kujifungulia nyumbani kwa wakunga wa jadi imeanza kutokomea, huku akiwahimiza wanawake wote kuendelea kuzingatia huduma za afya zinazotolewa katika vituo vya serikali. 

Sauti ya Mratibu wa huduma za mama na mtoto Bi Prisca John
Kipindi cha Ijue Halmashauri Yako kikiendelea katika studio za Redio Jamii Kilosa

Naye Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto (RCH) Bi Salma Kimwaga amesisitiza umuhimu wa kina mama wajawazito kuhudhuria kliniki kwa wakati ili afya zao na za watoto wao ziweze kufuatiliwa mapema.

Sauti ya Mratibu wa RCH Kilosa Bi Salma Kimwaga

Kwa upande wake, Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, Bi. Joyna Mlwale, amewataka waume kushiriki kwa karibu katika safari ya ujauzito kwa kuwasindikiza wake zao kliniki pamoja kuaanda usafiri wa dharula na fedha kwa mahitaji yatakayohitajika.

Sauti ya Afisa Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya wilaya ya Kilosa Bi Joyna Mlwale