Radio Jamii Kilosa

Vigodoro vyatajwa chanzo cha ukatili Kilosa

27 November 2025, 11:24 am

Maafisa Ustawi wa jamii wakiwa katika kipindi maalumu Redio Jamii Kilosa. Picha na Asha Madohola

Kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 Dunia hufanya kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia lengo likiwa ni  kupinga ukatili na kutetea haki za wanawake na watoto ambao wamekua wahanga wakubwa wa kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

Na Aloycia Mhina

Wazazi na walezi wilayani Kilosa wametakiwa kuwa makini na kulinda watoto wao dhidi ya mazingira hatarishi yanayochangia vitendo vya ukatili, ikiwemo muziki wa vigodoro ambao umeelezwa kuwa chanzo kikuu cha manyanyaso na ukatili kwa watoto.

Wito huo umetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, John Mpogole, katika mahojiano maalum kupitia kipindi cha Mambo Mseto kinachorushwa na Redio Jamii Kilosa, tarehe 24 Novemba 2025.

Mpogole alisema kuwa katika kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, ambazo huadhimishwa kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10, jamii inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha watoto hawashiriki wala kuingizwa kwenye sherehe za vigodoro, kwani maeneo hayo yamekuwa vyanzo vya ukatili wa kijinsia huku akiwashauri wazazi kufuatilia watoto wao katika shule za awali (day care), ili kuhakikisha wanalelewa katika mazingira salama na yanayozingatia maadili.

Sauti ya Afisa Ustawi wa Jamii Kilosa John Mpogole akizungumza

Katika hatua nyingine, Mpogole aliwataka wanawake kukataa vitendo vya udhalilishaji, ikiwemo kulazimishwa ngono kinyume na maumbile ndani ya ndoa, akibainisha kuwa wanawake wengi wamekuwa wakinyamazia ukatili huo kwa hofu au aibu ambapo alisisitiza kuwa ni muhimu kutoa taarifa kwa namba ya dharura 116 au kwa viongozi wa ngazi ya kijiji na kata ili hatua zichukuliwe.

Sauti ya Afisa Ustawi wa Jamii Kilosa John Mpogole akizungumza
Maafisa Ustawi wa Jamii wilayani wakitoa elimu kuhusu siku 16 za kupinga ukatili

Kwa upande wake, Mratibu wa shule za awali (day care) Wilaya ya Kilosa, Sylvester William Katikaza, amewahimiza wazazi kuhakikisha shule wanazowapeleka watoto wao zimesajiliwa rasmi na zina walimu wenye mafunzo sahihi ya malezi. Amesema baadhi ya shule zimekuwa zikiendeshwa bila kufuata viwango vya ubora, hivyo kuhatarisha ustawi wa watoto.

Sauti ya Mratibu wa shule za awali Sylivester Katikaza akizungumza

Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku 16 za kupinga ukatili ni “Tuungane Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia Mtandaoni”, ikisisitiza pia mapambano dhidi ya ukatili unaofanyika kupitia mitandao ya kijamii. Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa inaendelea na kampeni ya kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha watoto na wanawake wanalindwa ipasavyo.