Radio Jamii Kilosa

Wafanyabiashara Kilosa walia na ukosefu wa choo

24 October 2025, 7:52 pm

Muonekano wa soko la kilabu cha Mtendeni kwa sasa ambapo wafanyabiashara wanahitaji uwepo wa choo. Picha na Beatrice Majaliwa

Soko hilo la Kilabu cha Mtendeni linahudumia watu wengi kila siku, na bila choo, mazingira yameanza kuwa hatarishi kwa kusababisha uchafuzi unaoweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

Na Beatrice Majaliwa

Wafanyabiashara wa soko la kilabu cha Mtendeni lililopo katika Kata ya Mkwatani, Wilaya ya Kilosa, wameelezea hofu yao juu ya ukosefu wa huduma ya choo katika eneo hilo la biashara, hali ambayo wamesema imekuwa kero kubwa na inaweka maisha yao kwenye hatari ya kiafya.

Mfanyabiashara wa soko la Kilabu cha Mtendeni BiTukae Salumu Lutumbo

Wakizungumza na Redio Jamii Kilosa, iliyofika sokoni hapo kujione hali halisi wafanyabiashara hao akiwemo Bi. Tukae Salumu Lutumbo na Bw. Juma Ponela walisema kuwa mara nyingi wamejikuta wakikosa hifadhi ya heshima wanapohitaji huduma ya choo kwa haraka, huku wengine wakilazimika kuingia kwenye maeneo ya jirani na kuwasumbua wakazi wa maeneo hayo kwa sababu ya kukosa sehemu rasmi ya kutolea haja.

Mfanyabiashara wa soko la Kilabu cha Mtendeni BiTukae Salumu Lutumbo akizungumza
Mfanyabiashara Bw. Juma Ponela

Bw. Juma Ponela alisema kuwa hali hiyo si tu inaleta usumbufu, bali pia ni tishio kwa afya zao na ya wateja wao na kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta choo, jambo ambalo limesababisha usumbufu mkubwa kwao hasa wakati wa kazi za kila siku.

Sauti ya mfanyabiashara Bw. Juma Ponela akizungumza
Afisa Afya wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kilosa, Bw. Mark Saimon Kimaro

Akijibu malalamiko hayo, Afisa Afya wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kilosa, Bw. Mark Saimon Kimaro amesema kuwa tayari idara yake imefuatilia kwa karibu changamoto hiyo na mipango ya ukarabati wa choo katika soko hilo ipo mbioni kutekelezwa. Ameeleza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa miundombinu ya afya katika maeneo ya biashara, na juhudi zinafanyika kuhakikisha wafanyabiashara hao wanapata huduma hiyo muhimu.

Afisa Afya wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kilosa, Bw. Mark Saimon Kimaro akizungumza

Aidha, Bw. Kimaro amewataka wafanyabiashara wote katika maeneo ya masoko kuzingatia usafi wa mazingira yanayowazunguka kama sehemu ya kuhakikisha wanavutia wateja, lakini pia kulinda afya zao. Amehimiza ushirikiano baina ya wafanyabiashara na Serikali kuhakikisha mazingira bora ya biashara yanaimarika kwa manufaa ya wote.

Afisa Afya wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kilosa, Bw. Mark Saimon Kimaro akizungumza
Muonekano wa kilabu cha Mtendeni