Radio Jamii Kilosa

Kilosa yaimarisha usawa wa kijinsia

26 September 2025, 4:50 pm

Benjamin Elia Mang’ara,  Mratibu wa Program ya Kizazi chenye Usawa(GEF) akiwa katika studio za Redio Jamii Kilosa. Picha na Kadewele Said

Programu ya Kizazi chenye Usawa ni programu inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii, yenye lengo la kuhimiza usawa wa kijinsia katika nyanja zote za kijamii na kiuchumi na Programu hii inalenga kuwezesha wanawake kwa kuhakikisha wanapata huduma bora, wanamiliki ardhi na rasilimali, wanashiriki kwenye shughuli za uzalishaji, na mazingira ya kazi yanakuwa rafiki kwao na pia inahamasisha kubadilika kwa sera, sheria na mipango ya maendeleo ili kumpa mwanamke nafasi sawa na mwanaume.

Na Aloycia Mhina

Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imeendelea kuhimiza usawa wa kijinsia kwa kutekeleza kikamilifu Programu ya Kizazi Chenye Usawa, inayolenga kuhakikisha jamii inatambua kuwa watu wote ni sawa, pasipo ubaguzi wa kijinsia, hasa kwa wanawake.

Wito huo ulitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo Bw. Benjamini Mang’ara, ambaye pia ni Mratibu wa Programu hiyo, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Ijue Halmashauri Yako kinachorushwa na Redio Jamii Kilosa.

Benjamin Elia Mang’ara,  Mratibu wa Program ya Kizazi chenye Usawa akiwa na mtangazaji kwenye kipindi maalumu

Bw. Mang’ara amesema kuwa Halmashauri ya Kilosa imejiwekea vipaumbele vinne vya utekelezaji wa programu hiyo, ambavyo ni pamoja na kuboresha huduma za umma na sekta binafsi zinazolenga jinsia, kurasimisha kazi zisizo na malipo, pamoja na kuunda mazingira wezeshi ya kisera kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kukuza kazi zao.

Aidha, ameeleza kuwa halmashauri inalenga kuongeza upatikanaji wa ardhi na huduma za kifedha kwa wanawake ifikapo mwaka 2025/2026, sambamba na kuandaa mipango ya kiuchumi inayoendana na jinsia.

Katika hatua nyingine, Bw. Mang’ara amebainisha kuwa tangu mwaka 2021 hadi 2025, halmashauri imefanikiwa kutoa hati mbalimbali za umiliki wa ardhi kwa wanawake, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kumiliki rasilimali. Hili limekuwa ni jukumu muhimu katika kuhakikisha wanawake wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii.

Sauti ya Benjamin Elia Mang’ara,Mratibu wa Program ya Kizazi chenye Usawa akizungumza

Kwa upande mwingine, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imetekeleza maelekezo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha maeneo ya kazi yanakuwa rafiki kwa wanawake, ikiwemo kuwepo kwa vyumba maalum vya kunyonyeshea watoto kwa wanawake wanaonyonyesha na hatua hii ni sehemu ya kuhakikisha kuwa wanawake wanatekeleza majukumu yao ya kazi bila vikwazo, na pia inalenga kuinua ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.