Radio Jamii Kilosa

Wanachama 2,590 waandikishwa ICHF 2025 Kilosa

17 September 2025, 9:16 am

Mratibu wa CHF ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kilosa Elistone Elibahati.Picha Aloycia Mhina

Kwa mujibu wa takwimu, katika mwaka wa fedha 2024/2025 wanachama 15,000 waliandikishwa kwenye mfuko wa bima ya afya ICHF wilayani Kilosa na tangu kuanza kwa mwaka wa fedha huu wa 2025, hadi sasa, wanachama 2,590 tayari wamejiunga na kupatiwa kadi za ICHF.

Na Aloycia Mhina

Jamii wilayani Kilosa imetakiwa kuwa na mwamko wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (ICHF) iliyoboreshwa, ili kujihakikishia huduma bora za afya kwa kipindi cha mwaka mzima bila kulazimika kulipa fedha taslimu pindi wanapougua.

Rai hiyo ilitolewa, na Mratibu wa ICHF ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kilosa Elistone Elibahati, wakati akizungumza na Redio Jamii Kilosa kupitia kipindi cha Ijue Halmashauri Yako.

Afisa huyo alieleza kuwa kwa gharama ya shilingi 30,000 tu, kaya yenye watu sita inapata kadi ya CHF inayowaruhusu kupata huduma za matibabu kwa mwaka mzima katika vituo vya afya vya serikali vilivyosajiliwa.

Alisisitiza kuwa huduma hiyo ni muhimu hasa kwa watu wa kipato cha chini ambao mara nyingi hupata changamoto kubwa ya kugharamia matibabu pindi wanapougua.

Aidha, Mratibu huyo ametoa wito kwa wananchi kujiunga mapema na pia kuhakikisha wanafanya uhakiki wa kadi zao kabla hazijaisha muda wake pia akiwataka waandikishaji wa ICHF kwenye ngazi za vijiji na kata kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima hiyo.

Sauti ya Mratibu wa ICHF ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kilosa Elistone Elibahati, wakati akizungumza