Radio Jamii Kilosa

HESLB yatoa elimu ya mikopo kwa wanafunzi wa sekondari Kilosa

31 July 2025, 8:21 pm

Wanafunzi wakipatiwa elimu ya mikopo na Afisa mikopo kutoka bodi ya mikopo Tanzania Bi Farida Mwasse. Picha na Asha Madohola

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ina jukumu la kuhakikisha vijana wengi zaidi wa Kitanzania wanapata fursa ya kujiendeleza kielimu kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu. Vigezo vya kupata mkopo ni pamoja na ufaulu wa masomo, uhitaji wa kifedha, na kuchaguliwa kujiunga na taasisi ya elimu ya juu inayotambulika na mikopo hutolewa kwa kipaumbele kwa masomo ya sayansi, afya, elimu na fani nyingine muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Na Asha Madohola

Wanafunzi wakifuatilia mafunzo ya mkopo

Katika juhudi za kuwaandaa wanafunzi kwa maisha ya baada ya shule, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB na wamiliki wa vituo vya huduma ya maandiko (stationery), imeendesha mafunzo maalum kwa wanafunzi wa shule za sekondari Mazinyungu, Mbumi, Kutukutu na Dendego, yaliyofanyika jana katika shule ya sekondari Mazinyungu, wilayani Kilosa.

Afisa Mikopo kutoka HESLB, Bi Farida Mwasse, aliwafundisha wanafunzi hao kuhusu hatua za kuomba mkopo wa elimu ya juu, masharti ya kupata mkopo, pamoja na faida zake  huku akibainisha kuwa mikopo hiyo inalenga kusaidia wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kupata elimu ya juu kwa urahisi.

Sauti ya Afisa Mikopo kutoka HESLB Bi Farida Mwasse akizungumza

Kwa upande wake, Bi Graciana Mwinuka kutoka HESLB aliwaeleza wanafunzi kuwa kupata mkopo si tiketi ya ajira moja kwa moja, bali ni nyenzo ya kujiendeleza kielimu na kiujuzi na kusisitiza mkopo lazima ulipwe hata kama mhitimu hajapata ajira rasmi, hivyo aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili wafanikishe ndoto zao, hasa wale wanaosomea masomo ya sayansi waliotajwa kuwa na kipaumbele.

Sauti ya Afisa mikopo kutoka bodi ya mikopo Bi Graciana Mwinuka akizungumza

Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Bi. Milandu Kinyonga, alipongeza juhudi za serikali kupitia HESLB kwa kuwafikia wanafunzi wa vijijini na kwamba ushiriki wa wafanyakazi wa stationaries katika mafunzo hayo ni wa muhimu kwani huwasaidia wanafunzi katika maandalizi ya nyaraka sahihi za kuomba mkopo.

Sauti ya Afisa Elimu sekondari Bi Milandu Kinyonga akizungumza

Mwalimu Mkuu wa shule ya Mazinyungu, Mwl. Masegese Robert, alitoa shukrani kwa HESLB kwa kutoa elimu hiyo muhimu kwa wanafunzi, kwani yamewaamsha wanafunzi kuelewa namna wanavyoweza kusonga mbele kielimu bila kikwazo cha kifedha.

Sauti ya Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Mwl Masegese Robert

Kupitia mafunzo hayo, wanafunzi  akiwemo Sadamu Augustino na Josephine Mlossa wameonyesha kufurahia elimu waliyoipata na kueleza kuwa sasa wana uelewa mpana kuhusu mchakato wa mikopo ya elimu ya juu na namna ya kujiandaa kimasomo ili kupata fursa hiyo muhimu ya kujikwamua kielimu na kiuchumi.

Sauti ya wanafunzi Josephine Mlosa akizungumza