Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
3 July 2025, 3:21 pm

Afya ya akili ni hali ya ustawi wa kiakili, kihisia na kijamii inayomuwezesha mtu kukabiliana na changamoto za maisha, kufanya kazi kwa ufanisi, na kuchangia katika jamii matatizo ya kiafya. Afya ya akili inahitaji uangalizi sawa na afya ya mwili, na jamii inapaswa kuepuka unyanyapaa kwa watu wenye changamoto hizo ili kuwasaidia kupata tiba na msaada stahiki.
Na Aloycia Mhina
Vijana wilayani Kilosa wamezungumza kwa nyakati tofauti na Redio Jamii Kilosa wakieleza umuhimu wa afya ya akili kwa vijana na jamii kwa ujumla, wakisisitiza kuwa changamoto za afya ya akili zimekuwa zikiwakumba vijana wengi kutokana na msongo wa mawazo, ukosefu wa ajira, na matatizo ya kifamilia.
Bernad Semwenda alisema kuwa wengi wa vijana hukumbwa na changamoto hizo lakini hukosa sehemu ya kuzungumzia matatizo yao kwa hofu ya kuhukumiwa au kutoeleweka, jambo linalochangia kuongezeka kwa matatizo ya akili katika jamii.

Naye, Abdulatifu Wasiwasi aliihimiza serikali kupitia Wizara ya Afya na elimu kutoa elimu ya mara kwa mara kuhusu afya ya akili mashuleni, vyuoni na kwenye jamii ili kuwasaidia watu kutambua dalili mapema na kuwahamasisha wanaokumbwa na changamoto hizo kutafuta msaada wa kitaalamu.

Kwa upande wake Mtaalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, Dkt Edwin Baraza, aliitaka jamii kuacha tabia ya kuwadharau, kuwacheka au kuwafungia ndani watu wenye matatizo ya afya ya akili, badala yake wawasaidie kufika hospitali ili wapate matibabu.
“Baadhi ya familia hufikia hatua ya kuwafungia wagonjwa hao ndani kwa madai kuwa ni “wasumbufu” jambo ambalo ni kinyume na haki za kibinadamu na wapo wagonjwa wa afya ya akili wanaoonekana kama chanzo cha aibu na hivyo hufichwa hii si sahihi tuwasaidie, kwani afya ya akili inatibika,” alisema Dkt Baraza.