Radio Jamii Kilosa

Karafuu kuwa mkombozi wa chakula shuleni

12 May 2025, 2:09 pm

Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wilaya ya Kilosa Elia Shemtoi akiwa katika kikao cha lishe. Picha na Asha Madohola

Suala la lishe nchini limekuwa ni tatizo kubwa ambalo serikali imejizatiti ili kuondoa kadhia hiyo ambayo imekuwa ikisababisha wananchi kupata matatizo ya kiafya kutokana na kukithiri kwa lishe duni .

Na Asha Madohola

Katika kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula cha mchana shuleni na kuboresha lishe, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imepokea miche 16,000 ya karafuu ambayo imesambazwa kwenye baadhi ya shule wilayani hapa.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa kikao ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Ndg. Elia Shemtoi, ambapo ameeleza kuwa baada ya miaka minne, shule hizo zitaanza kuvuna mazao hayo na kupata fedha zitakazosaidia kununua chakula kingi kwa ajili ya wanafunzi.

Kikao hicho cha kupitia mpango na matumizi ya fedha za lishe kwa mwaka 2024/2025, hususan kwa robo ya tatu, kilifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ambapo mwenyekiti huyo aliwasihi wazazi kutambua umuhimu wa lishe kwa watoto na kuchangia chakula shuleni.

Sauti ya Kaimu Mkurugenzi Ndg Elia Shemtoi
Afisa lishe wilaya Kilosa ndg Elisha Kingu

Akizungumza katika kikao hicho, Mratibu wa Lishe wa Wilaya ya Kilosa, Ndg. Elisha Kingu, ameeleza kuwa licha ya asilimia 87.6 ya shule wilayani humo kutoa chakula shuleni, bado kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaokosa mlo wa mchana na kwamba hali hiyo inatokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo uelewa mdogo wa wazazi kuhusu umuhimu wa kuchangia chakula shuleni.

Sauti ya Afisa lishe Ndg Elisha Kingu
Afisa elimu msingi Ndg Richard Mpumilwa

Kwa upande wao, Maafisa Elimu wa Msingi na Sekondari wamekiri kuwepo kwa changamoto hiyo, wakieleza kuwa baadhi ya wazazi hawajitokezi kuchangia chakula kwa watoto wao na kwamba baada ya msimu wa mavuno, wanatarajia idadi ya watoto wanaopata chakula shuleni itaongezeka.

“Kuna umuhimu mkubwa sana wa wanafunzi kupata chakula cha mchana shule kwa sasa tunaendelea kuwapatia wanafunzi wenye madarasa yenye mitihani lakini baada ya mavuno wote watapata chakula kwa kuwa mavuno yatakuwa mengi na wanaendelea kuwahamasisha wazazi kushiriki katika kuchangia kwa kuwa linawahusu”. amesema Afisa elimu Richard

Sauti ya afisa elimu msingi na sekondari

Afisa Kilimo wa Wilaya ya mifugo, Bi. Faraja Jofrey Sanga, alihimiza shule zinazomiliki maeneo ya kilimo kutumia fursa hiyo kulima mazao mbalimbali na kupanda bustani za mboga mboga.

Sauti ya Afisa kilimo Bi Faraja Sanga