Wazazi Kilosa waelimishwa kuhusu umuhimu wa elimu jumuishi kwa watoto wenye ulemavu
4 December 2024, 8:18 pm
Katika muendelezo wa siku 16 za kupinga ukatili duniani wilayani Kilosa Jeshi la Polisi kupitia dawati la jinsia na watoto kwa kushirikiana, dawati la msaada wa kisheria, Ustawi wa Jamii na Smaujata wameendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili kwa kuyagusa makundi ya wanawake na watoto.
Na Asha Madohola
Wadau wa elimu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kilosa wameendesha kampeni ya uhamasishaji katika Shule ya Msingi Kichangani, wakitoa elimu kwa wazazi kuhusu umuhimu wa elimu jumuishi kwa watoto wenye ulemavu.
Kampeni hiyo iliyofanyika leo 04 Disemba 2024 shuleni hapo imelenga kuwahamasisha wazazi kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu wa umri wa miaka mitano hadi saba, ili kupata haki yao ya msingi ya elimu kama watoto wengine.
Koplo Hemed Rajabu Chabu kutoka Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto katika Jeshi la Polisi Kilosa amesema kuwa watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali, kama vile ualbino, usonji, uziwi, na matatizo ya kuona, wana haki ya kupata elimu bila ubaguzi.
Amewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha wanawapatia watoto hao nafasi ya kupata elimu, ambayo ni msingi wa maisha yao ya baadaye.
“Watoto wenye ulemavu wana haki ya kupatiwa elimu kama watoto wengine na sisi kama Jeshi la Polisi Kilosa tupo tayari kutoa ushirikiano wa ulinzi kwa watoto na hata watakaokuwa tishio basi watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na tunashukuru wazazi kwa kuhamasika na elimu hii” alisema Koplo Chabu.
Kampeni hiyo imewezeshwa kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali, zikiwemo Taasisi ya Elimu ya Msingi, Idara ya Ustawi wa Jamii, na Dawati la Msaada wa Kisheria. Wadau hao wameeleza kuwa lengo ni kubadili mtazamo wa jamii kuhusu watoto wenye ulemavu, kwa kuhakikisha wanapata fursa sawa katika elimu na maisha.
Wazazi waliohudhuria kampeni hiyo walionesha mwitikio chanya, wakieleza kufurahishwa na elimu waliyopewa. Hata hivyo, baadhi yao walilalamikia changamoto za kiuchumi, ambazo zinawafanya washindwe kumudu mahitaji ya msingi ya watoto wao wakiwa shuleni. Wadau wameahidi kuendelea kushirikiana na jamii kutafuta njia za kupunguza changamoto hizo, ikiwemo kutafuta ufadhili na misaada ya vifaa vya shule kwa watoto wenye ulemavu.
Kampeni hii imeibua matumaini mapya kwa wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu, huku ikisisitiza kuwa elimu ni haki ya kila mtoto ambapo wadau wa elimu wamewataka wazazi kushirikiana nao kikamilifu ili kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya kujiendeleza kupitia elimu jumuishi.