Radio Jamii Kilosa

Uboreshaji wa lishe kwa watoto wilayani Kilosa wapewa kipaumbele

20 November 2024, 11:17 pm

Kushoto ni Katibu Tawala wilaya ya Kilosa Ndg Salome Mkinga, na DMO Dr. Seleman Kasugulu wakifuatilia kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe robo ya kwanza. Picha na Eliza Makemba

Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa inaendelea kutekeleza afua mbalimbali za Lishe kwa kuzingatia viashiria vya Mkataba wa Lishe kwa kushirikiana na Watendaji wa Kata na Vijiji, Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii na watoa Huduma za Afya vituoni, kwa lengo la kuboresha na kuimarisha afya na Lishe ya watoto, vijana balehe, wajawazito,wanaonyonyesha na wanawake waliopo katika umri wa kuzaa.

Na Asha Rashid Madohola

Katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe robo ya kwanza kuanzia Julai-Septemba 2024 kilichofanyika leo 20 Novemba 2024 katika ukumbi wa Maktaba ya Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, viongozi wa wilaya waliweka mkazo mkubwa kwenye juhudi za kuboresha lishe ya watoto.

Katibu Tawala wa Wilaya, Ndugu Salome Mkinga, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, alisisitiza umuhimu wa lishe bora katika ustawi wa watoto.

“Watoto ni msingi wa taifa letu. Tusipowekeza kwenye afya na lishe yao leo, tunahatarisha kesho yetu,” alisema Mkinga huku akihimiza hatua za haraka kuhakikisha watoto wanapata chakula chenye virutubishi.

Sauti Das Kilosa akizungumza
Watendaji kata wakifuatilia kikao kazi

Aidha Mkinga aliwataka maafisa afya kushirikiana na viongozi wa vijiji kutoa elimu ya lishe kwa wananchi na elimu hiyo itasaidia kuwahamasisha wazazi na wanajamii kuchangia chakula kwa ajili ya watoto walioko shuleni.

“Takwimu zinaonesha hali ya lishe kwa watoto si nzuri. Tunapaswa kuhakikisha kila mtoto anapata chakula bora shuleni,” aliongeza.

Sauti ya Das Kilosa Ndg Salome akizungumza
Afisa Lishe wilaya ya Kilosa Ndg Elisha Kingu

Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Wilaya, Ndugu Elisha Kingu, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa robo ya kwanza ambapo alisema kuwa changamoto kubwa ni idadi ndogo ya watoto wanaopata chakula shuleni pamoja na uhaba wa viwanda vya kuongeza virutubishi kwenye vyakula.

“Tumeamua kuwekeza zaidi katika elimu ya lishe kwa wajasiriamali wa vyakula shuleni na kushirikiana na jamii kuhakikisha mabadiliko chanya,” alisema Kingu.

Mtendaji kata ya Mabula Ndg Emmanuel Solomon

Watendaji wa kata waliohudhuria kikao hicho walieleza dhamira yao ya kushirikiana na wazazi na kamati za shule ili kuhakikisha chakula kinapatikana kwa watoto shuleni.

“Kazi yetu ni kuunganisha nguvu na jamii. Tumejipanga kuhakikisha watoto hawakosi chakula shuleni ili kupunguza tatizo la utapiamlo,” alisema mmoja wa watendaji hao.

Sauti ya Mtendaji wa Mabula akizungumza
Mtendaji wa kata ya Lumuma Ndg Sabbath Malegesi
Sauti ya Mtendaji Lumuma akizungumza