Kilosa yajipanga kuadhimisha siku ya lishe Kitaifa
11 October 2024, 2:16 pm
Suala la udumavu na utapiamulo nchini bado ni changamoto kubwa katika baadhi ya maeneo hapa nchini ambapo katika kukabiliana na kadhia hiyo serikali imeendelea kutoa elimu ya lishe bora kwa wazazi na walezi ambao ndio wanajukumu la kuhakikisha wanawahudumia watoto kwa kuzingatia mlo kamili.
Na Asha Rashid Madohola
Wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha wanahudhuria kliniki kwa kipindi chote cha makuzi ya mtoto cha siku elfu moja ili kuweza kubaini maendeleo yake ya ukuaji na kubaini kama ana tatizo la udumavu ama utapiamulo aanze kupatiwa huduma mapema.
Hayo yalibainishwa na Winfrida Nkoba Afsa Tabibu wilaya ya Kilosa ambaye anafanya kazi katika zahanati ya Msowero wakati akizungumza na Redio Jamii Kilosa katika kuelekea maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa ambapo kiwilaya yataadhimishwa katika kata ya Msowero na kusema kuwa katika siku hiyo watatoa huduma ya mama na mtoto kwa kubaini uwepo wa tatizo la udumavu na utapiamulo kwa watoto.
Naye Kaimu Mtendaji kata ya Msowero George Mbogo alisema kuwa wapo kama wenyeji wapo tayari kuyapokea maadhimisho hayo ambapo ameishukuru serikali kuwapelekea maadhimisho hayo katika kata yao ambayo yatakuja chachu ya utoaji elimu ya lishe kwa wananchi ambao asilimia kubwa ni wakulima na wafugaji.
Kwa upande wake Afsa Lishe Ndg Elisha Kingu alisema wamejipanga vizuri kuadhimisha siku ya lishe katika kata ya Msowero kwa lengo la kutoa elimu ya lishe na mtindo bora wa maisha kwa wananchi ili kuweza kujikinga na maradhi ya utapiamulo ambalo limekua tatizo kwa watoto na watu wazima.
“Nitoe hamasa kwa wananchi wa wilaya ya Kilosa kuendelea kupata lishe bora na sahihi kwa watoto wadogo, vijana, rika la kati na wazee lakini pia tukumbuke lishe sahihi ni mlo wenye virutubisho sahihi ambavyo haviwezi kuharibu afya ya mtu” alisema Afsa Lishe.
Hata hivyo Afsa Lishe Kingu alisema utapiamulo mkali unaweza kupelekea kifo hivyo ameishauri jamii kuwahi kufika Hospitali mapema kwa ajili ya kupatiwa matibabu huku akiitaka jamii kuzingatia wanachokula pamoja na kufanya mazoezi ili kuepukana na maradhi hayo.
Siku ya lishe kitaifa huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 30 ya kila mwaka na katika mwaka huu 2024 maadhimisho hayo yamebebwa na kaulimbiu isemayo ” Mchongo ni afya yako zingatia unachokula”.