Radio Jamii Kilosa

Waganga wafawidhi Kilosa watakiwa kusimamia ukusanyaji mapato

13 September 2024, 11:23 pm

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Ndg Michael Gwimile akiwa katika kikao kazi na waganga Wafawidhi Kilosa. Picha na Kitengo cha mawasiliano serikalini

Serikali imedhamiria kupambana na changamoto zinazoikabili sekta ya afya kwa kuwatumia waganga Wafawidhi kuimarisha maadili kwa watumishi vituoni na usimamizi wa mapato ili wateja ambao ni wananchi waweze kufurahia huduma bora.

Na Asha Madohola

Waganga Wafawidhi Wilayani Kilosa wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili waweze kuboresha utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mhe. Wilfred Sumari wakati akizungumza na Waganga Wafawidhi katika kikao cha kuwajengea uwezo waganga hao kilichofanyika Septemba 13, 2024 katika ukumbi wa Maktaba ya Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Mhe Wilfred Sumari akiwa katika kikao kazi na waganga Wafawidhi Kilosa. Picha na Kitengo cha mawasiliano serikalini

Mhe. Sumari aliwataka Waganga hao kufanya kazi kwa ushirikiano na kusaidiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Serikali ya awamu ya sita imeleta fedha nyingi katika Halmashauri ya wilaya ya Kilosa kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo sasa kuna haja ya kushirikisha ngazi zote za uongozi kuanzia uongozi wa kijiji na wataalamu wote katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan miradi ya afya ili iweze kukamilika kwa wakati na kukidhi mahitaji ya wananchi” alisema Mhe Sumari.

Sauti ya Mhe Sumari
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Ndg Michael Gwimile

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Michael J Gwimile aliwataka Waganga Wafawidhi wa vituo kusimamia suala zima la ukusanyaji wa mapato kwa kuwa ni wajibu wa kila mtumishi kushiriki katika kukusanya mapato.

“Lakini vema pia tukashirikiana katika changamoto mbalimbali zinazojitokeza ili ziweze kutatuliwa kwa wakati ili kuboresha na kutoa huduma bora kwa wananchi katika sekta hii ya afya”alisema Mkurugenzi Gwimile.

Sauti ya Mkurugenzi Ndg Gwimile
Waganga Wafawidhi wakifuatilia kikao kazi