TFRA yazindua kampeni ya kilimo ni mbolea Kilosa
4 September 2024, 12:54 pm
Ili kuikuza sekta ya kilimo pamoja na kuhakikisha wakulima wanapata tija katika kilimo kwa kujikwamua kiuchumi, serikali imekuja na mpango wa kuwasajili wakulima katika mfumo wa kidijitali utakaowawezesha kupata ruzuku ya mbolea.
Na Asha Madohola
Wito umetolewa kwa wakulima wa wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kujisajili katika mfumo wa kidijitali ili waweze kunufaika na mpango wa mbolea ya ruzuku unaotolewa na serikali kwa wakulima ili waweze kununua mbolea kwa bei nafuu.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania TFRA Bi. Elizabeth Bolle katika hafla ya ufunguzi wa kampeni ya kilimo ni mbolea yenye kaulimbiu “Ongeza mavuno kwa matumizi sahihi ya mbolea” iliyofanyika viwanja vya shule ya msingi Kilosa Town.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mhe. Wilfred Sumari amewakumbusha wakulima kufuata kanuni bora za kilimo ambazo huanzia kwa kuchagua eneo sahihi kwa ajili ya zao litakalopandwa, kuandaa shamba kwa wakati na kuchagua mbegu bora iliyothibitishwa na wataalam wa kilimo.
“Niwashauri wakulima mnatakiwa kuhakikisha mnapanda kwa wakati sahihi, mnatumia mbolea kwa wakati na mbolea sahihi pia kupalilia kwa wakati sahihi na kuvuna kwa wakati, kwa kufanya hivyo itakusaidia kupata mazao mengi kwa ajili ya chakula au biashara” alisema Mwenyekiti Sumari.
Kwa Upande wake Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wilayani Kilosa Elia Shemtoi amesema kuwa wataendelea na kampeni hiyo kama idara huku akiwaasa wakulima kutunza namba za usajili na wakati wa kununua wakafanye manunuzi kupitia simu zao.
“Nawasisitiza nendeni mkatumie mbolea kwa kipimo sahihi kama mnavyoelekezwa na serikali msizidishe mbolea kwani itakuwa sumu kwenye udongo ” amesema Shemtoi
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilosa Bi. Salome Mkinga akiwa amekaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa amewaasa wakulima kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali ikiwa ni pamoja na kupata mbolea ya ruzuku ambayo itaisaidia serikali kupata takwimu sahihi zitakazotumika kuwasaidia wakulima kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kupata huduma kama vile ugani, taarifa za masoko na huduma za kifedha kupitia mfumo wa kanzidata ya usajili.