Loliondo FM
Loliondo FM
10 November 2026, 7:29 am

Watu watatu wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa kufuatia ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Esirwa, Kijiji na Kata ya Endulen, Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha.
Na Saitoti Saringe
Ajali hiyo imetokea Novemba 9, 2026, majira ya saa kumi jioni, ikihusisha gari aina ya Land Rover lenye namba za usajili T 227 AZJ, lililokuwa likisafiri kutoka Karatu kuelekea Endulen.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, gari hilo lilipata hitilafu katika mfumo wa breki na kupinduka, na kusababisha vifo vya watu watatu papo hapo, ambao ni wanaume wawili na mwanamke mmoja.
Aidha, watu saba wamejeruhiwa katika ajali hiyo, wakiwemo wanaume wanne, wanawake wawili na mtoto wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Majeruhi wote wamefikishwa katika Hospitali ya Endulen kwa ajili ya matibabu, huku miili ya marehemu ikihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo.
Akitoa pole kufuatia ajali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Luteni Kanali Robert Augustino Kakomangile, amewapa pole ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu kwa kuondokewa na wapendwa wao, huku akiwatakia majeruhi wote nafuu ya haraka.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na tahadhari za usalama barabarani, ikiwemo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vya usafiri ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.