Loliondo FM

Aweso atoa miezi mitatu kukamilisha mradi wa maji wa vijiji nane Loliondo

30 September 2026, 11:02 pm

Waziri wa maji mhe Juma Aweso akizungumza na wananchi alipotembelea mradi wa maji Loliondo. Picha na Saitoti Saringe

Na, Saitoti Saringe

Waziri wa Maji, Juma Aweso, amewataka watendaji wa Wizara ya Maji, RUWASA na AUWSA kuhakikisha kuwa ndani ya miezi mitatu Mradi wa Maji wa Vijiji Nane Loliondo unakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wapatao 30,000.

Waziri Aweso ametoa agizo hilo baada ya kutembelea eneo la mradi na kukagua maendeleo ya utekelezaji wake, ambapo amesisitiza kuwa changamoto ya wananchi kukosa huduma ya maji haipaswi kuendelea kuwa jambo la kawaida.
Amesema jukumu la Wizara ya Maji ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa wakati, huku akiwataka watendaji kutokuzoea changamoto zinazowakabili wananchi.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa vyanzo vya maji katika maeneo ya Orkanjoro na Yasi, matanki tisa ya maji, ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 82, ujenzi wa vituo vya maji 64, mabauti 11, pamoja na ununuzi na ufungaji wa pampu.
Kwa sasa, mradi huo umepokea zaidi ya shilingi bilioni 3.5 na utekelezaji wake umefikia takribani asilimia 60.

Kati ya kilomita 82 za mabomba zinazotarajiwa kulazwa, kilomita 15 tayari zimekwishalazwa, huku Tenki Kuu la Ngarwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni moja za maji likiwa limefikia takribani asilimia 90 ya ujenzi.

Waziri Aweso amesema atarejea Loliondo baada ya miezi mitatu kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo, akisisitiza kuwa kwa sasa wananchi wanachohitaji ni maji na si maelezo zaidi.

Sauti ya mheshimiwa Juma Aweso Waziri wa Maji