Loliondo FM

Ngorongoro yatakiwa kujiandaa kukabiliana na mabadiliko ya sera, mtaala wa elimu

29 August 2026, 10:31 am

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro wakishiriki katika kikao cha Baraza la Madiwani, kilichojadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya Halmashauri.

Afisa Elimu Mkoa wa Arusha, Dkt. Vincent Kayombo, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kujiandaa kikamilifu kukabiliana na mabadiliko ya sera ya elimu na mtaala mpya, ikiwemo kuongeza miundombinu na nafasi za wanafunzi.

Na Zacharia Jemes

Akizungumza katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Agosti 27, 2026, Dkt. Kayombo amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 imefanyiwa maboresho na kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, hatua iliyokuja na mabadiliko katika mfumo wa utoaji wa elimu nchini.

Amesema miongoni mwa mabadiliko hayo ni kuimarishwa kwa elimu ya lazima hadi kidato cha nne, jambo ambalo linahitaji Halmashauri kujiandaa mapema kwa kuongeza miundombinu na kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

Dkt. Kayombo amesema changamoto kubwa inayohitaji maandalizi maalumu ni uwepo wa makundi mawili ya wanafunzi wanaotarajiwa kuingia kidato cha kwanza kwa wakati mmoja, kutokana na wahitimu wa darasa la sita na darasa la saba kuingia katika mfumo wa sekondari.

Amesema hali hiyo inahitaji maandalizi ya mapema ili kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayekosa nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi.

Aidha, Dkt. Kayombo amesema Mpango Mkakati wa Mkoa wa Arusha katika sekta ya elimu unalenga kushughulikia changamoto mbalimbali, ikiwemo kuimarisha ufaulu wa wanafunzi, na kuwataka madiwani kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utoaji wa elimu katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Manja Sironga Yaile, amesema Halmashauri imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na ongezeko la wanafunzi kwa kupanga kujenga shule mpya na kukamilisha zilizopo katika maeneo ya Oloipiri, Ololosokwan, Naan na Sibali.

Mhe. Yaile amesema ujenzi na ukamilishaji wa shule hizo unalenga kuongeza uwezo wa Halmashauri kupokea wanafunzi watakaohitimu darasa la sita na la saba kwa pamoja, huku akieleza kuwa lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2028 hakuna upungufu wa nafasi kwa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza.
Amesema hayo wakati akifungua kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Ameongeza kuwa, pamoja na ujenzi wa shule mpya, Halmashauri imepanga kukamilisha miundombinu mbalimbali ya elimu, ikiwemo maabara, madarasa, nyumba za walimu na miundombinu mingine wezeshi, ili kuongeza ubora wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Mhe. Yaile amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mikakati ya Halmashauri ya kuhakikisha mabadiliko ya sera na mfumo wa elimu yanaenda sambamba na upatikanaji wa miundombinu, nafasi za wanafunzi na mazingira bora ya elimu.

Kwa hatua hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro inalenga kujiandaa mapema na mabadiliko ya mfumo wa elimu, kuongeza uwezo wa kupokea wanafunzi na kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari.