Loliondo FM

Amuua mke wake, atokomea kusikojulikana

15 February 2024, 12:22 am

Picha na mtandao.

Matukio ya ukatili kwa wanawake hususani ya mauaji yameshamiri kwa mwezi Februari wilayani Ngorongoro ya wanaume kuwaua wake zao hili likiwa ni tukio la pili kwa mwanaume kumua mkewe ndani ya wiki moja tu.

Na Edward Shao.

Kijana mmoja anayejulikana kwa jina la Larinyoni Saitoti Parmeres (28) mkazi wa kijiji cha Lopuluni kitongoji cha Lopoluni A tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro anatuhumiwa kumuua mke wake Nang’obukule Ikayo Mbalala (20) kwa kumpiga na rungu maarufu namba tisa kichwani na kumkata na kitu chenye ncha kali maeneo mbalimbali ya mwili wake kisha kutokomea kusikojulikana

Akizungumza na Loliondo Fm mwenyekiti wa kijiji cha Lopoluni Bw. Daniel Kurtut amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jumatano ya Februari 14. 2024 ambapo mtuhumiwa baada ya kutenda ukatili huo alitoroka na wao kwa kushirikiana na jeshi la polisi watahakikisha anapatikana na kufikikishwa kwenye vyombo vya dola.

Sauti ya Mwenyekiti

Jitihada za kumtafuta kamanda wa polisi mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo kutaka kujua undani pamoja na chanzo cha mauaji hayo ziligonga mwamba kwani simu yake iliita bila mafanikio huku mtuhumiwa akiwa bado ajulikani alipo.

Hili ni tukio la pili kutokea wilayani hapa ndani ya wiki moja, kwani katika kijiji cha Malambo tarehe 06/02/2024 mwanaume mmoja kwa jina la Lanyori Mathayo (25) alimuua mke wake kwa kipigo baada ya kugoma kuishi nae.