Loliondo FM

Tatizo la umeme Ngorongoro

8 December 2023, 4:39 pm

Fundi wa shirika la umeme Tanesco akiwa katika majukumu yake Ngorongoro, picha na Saitoti Saringe

Wananchi wilayani Ngorongoro wamekuwa wakiitaja kero ya kukatika kwa umeme mara kwa mara kuwa ni moja ya kero kubwa kwao kwani wamekuwa wakiofia kuungua kwa mali zao zinazotumia umeme na hata kushindwa kufanya kazi zao za kila siku hususani wale wanaotumia nishati ya umeme katika majukumu yao ya kila siku.

Na Edward Shao

Mkuu wa wilaya ngorongoro Mwl Raymond Mwangwala akizungumza wakati wa kuitimisha kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya kilichofanyika hii leo 02 Novemba 2023 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri amesema wajumbe wameazimia kutatua changomoto ya kukatika kwa umeme inayowasumbua wananchi kwa kupeleka maombi kwenye kikao cha kamati ya ushauri mkoa kuyabariki ili kupata huduma ya umeme kutokea eneo la Engaruka kwani kwasasa wilaya inatumia umeme kutokea Longido ambapo umekuwa ukikatika mara kwa mara kufuatia umbali pamoja na matumizi makubwa huko unakotokea.

Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro mwalimu Raymond Mwangwala,picha na Saitoti Saringe

Sambamba na hayo katika kikao hicho kimetajwa baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo ambayo serikali imetoa fedha nyingi kwaajili ya utekelezwaji wilayani hapa ambayo ni pamoja na miradi mikubwa ya maji, afya ambapo wamepata vifaa tiba vya kutosha katika vituo vingi vya afya, na kwa upande wa elimu sekondari wakifanikiwa kupata madarasa,mabweni pamoja na madawati huku shule za msingi wakijengewa madarasa mapya na ujenzi wa shule mpya ya msingi Kirtalo.

Mkuu huyo wa wilaya ya Ngorongoro amewataka wananchi kuilinda miundombinu yote ya miradi ya maendeleo huku akitoa maagizo kwa kamati zote za maafa kila moja kusimama na kutekeleza majukumu  yao kipindi hiki cha mvua kuepusha maafa huku akiwataka wananchi wanaoshi mabondeni kuhamia sehemu salama ili kuweza kuepukana na maafa yatakayotokana na mvua.

Sauti ya mkuu wa wilaya mwalimu Raymond Mwangwala

Kwa upande wao viongozi wa kidini wamemshukuru mkuu wa wilaya kushirikishwa katika kikao icho cha ushari na kumpongeza Mh rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo pamoja na kuomba wananchi kuitunza miundombinu yote ya miradi ya maendeleo.

Sauti za viongozi wa dini

Kikao hicho cha kamati ya ushauri wilaya kilikuwa na lengo kuu la kusikiliza na kushauri kazi na miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali ya  Dk Samia Suluhu kikiwa na wajumbe ambao ni taasisi za umma,wakuu wa idara, watendaji wa kata,maafisa tarafa,viongozi wa dini,viongozi wa vyama vya siasa,kamati ya ulinzi na usalama,mkurugenzi akiwa ndiye katibu na mkuu wa wilaya ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo.